Kamanda wa Kikosi cha Usalama wa barabarani, Mohamed Mpinga 
Dar es Salaam.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama wa barabarani, Mohamed Mpinga amefunguka kwa kueleza anavyokwazwa na baadhi ya viongozi wa juu wa Serikali, wanavyokwamisha utendaji kazi wa askari wake.  

Kamanda Mpinga aliyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake, ambapo alibainisha kuwa vigogo hao wamekuwa wakiingilia utendaji kazi wa askari wake hasa wanapokamatwa ndugu zao kwa kukiuka sheria.

“Wapo wengi ambao husababisha Sheria za Usalama Barabarani kuvunjwa kwa makusudi na ndugu, jamaa au rafiki zao kwa kuwa watu hao mara wanapokamatwa, huwasiliana na vigogo hao kwa njia ya simu ambapo vigogo hao huanza kuwatisha askari wangu, pamoja na kuwalazimisha kutowachukulia hatua, “ alisema Mpinga.
Aliongeza:” Kwa kutambua hilo ndugu, jamaa na marafiki wa vigogo hao, wamekuwa wakikiuka sheria husika kusudi. Yaani mtu amegonga, unakuta kigogo anapiga simu kwamba asifunguliwe mashtaka, kwa kweli ni vyema kuongoza nchi kwa msingi wa sheria,” alisema Kamanda Mpinga huku akikunja uso kuonyesha kukerwa na jambo hilo.

Mpinga alisema hali hiyo ndiyo imesababisha nidhamu wanayopaswa kuwa nayo madereva barabarani kushuka hata kuamua kujiunga kwenye misafara ya viongozi mbalimbali, wakiwa na imani kwamba, hawawezi kuchukuliwa hatua kwa kuwa watakingiwa kifua na vigogo hao.
“ Nimewaeleza trafiki wote kuwa makini zaidi kwenye misafara, kwa sababu siku hizi hali imebadilika. Wawe wanajiangalia jinsi wanavyosimamia au kuongoza misafara wakizingatia na usalama wa maisha yao kwa jumla,” alisema Kamanda Mpinga.

“Hata hivyo, napenda kuwahakikishia kwamba nitasimamia sheria katika utendaji wangu wa kazi, simu ikipigwa kwangu sitoi ushirikiano wa aina hiyo. Nawasihi viongozi wenye tabia hizo waache kuingilia utendaji kazi wa askari, mtu anapita taa nyekundu inawaka akikamatwa lazima alipe faini,” alisema.

Aidha, alizungumzia kuhusu tuhuma zilizokuwa zikielekezwa kwa askari wake za kuwa na vitabu bandia vya kuandika adhabu, ambapo alieleza kuwa jambo hilo halina ukweli, huku akieleza kwamba vitabu vinavyotumika vilichapwa vingi mwaka 2011.

“Nimesikia tuhuma hizi, lakini nawahakikishia wananchi kwamba hazina ukweli kwa sababu baada ya kusikia nilifuatilia nikabaini hofu yao inatokana na mwaka kwa kuwa vitabu vingi vina GN 2057 2011 vilitolewa makao makuu ya polisi,” alifafanua Kamanda Mpinga.