Baadhi ya waombaji walioongea na gezeti hili walilalamikia kitendo hicho wakisema kinawasababishia usumbufu na kuwakwamisha katika kufanya.Uchunguzi wa gazeti hili unaonyesha kuwa baadhi ya wafanyakazi wa Idara ya Uhamiaji na vishoka, tayari wameanza kujinufaisha na tatizo hilo kwa kuomba rushwa kutoka kwa waombaji hati hizo ili wawatekelezee matakwa yao kwa haraka.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani Mbarak Abduwakil alikataa kuzungumzia suala hilo, akidai kuwa amebanwa na vikao ofisini kwake.Hata hivyo, Kaimu Ofisa Uhusiano wa Uhamiaji, Tatu Burhan alikiri kuwepo kwa tatizo hilo, lakini akasema halitokani na mashine zao kuharibika.
“Tatizo hili limetokana na ukosefu wa malighafi toka nje ya nchi. Unajua malighafi hizo tunaziagiza, lakini kwa bahati mbaya hazikuweza kupatikana kwa wakati,” alisema Tatu.
Pamoja na uhaba wa mali ghafi, alisema kwa bado Uhamiaji iliendelea kutoa pasipoti kwa wenye maombi maalumu ya dharura.Alikiri pia kwamba kwa waombaji wasio na dharura maombi yao yaliwekwa kando yakisubiri kuwasili kwa malighafi.
Hata hivyo Tatu alisema kuwa mali ghafi hizo zimeshawasili Bandari ya Dar es Salaam jana na walikuwa katika harakati za kuzitoa.
“Hivi ninavyozungumza (jana) malighafi ghafi hizo tayari zimefika bandarani na tupo kwenye harakati za kuzichukua,” alisema.
Alisema kuwa pamoja na malighafi hizo kuwasili ni vigumu kuchapisha pasipoti zote kwa wakati mmoja kutokana na wingi wa maombi.Hata hivyo alisisitiza kuwa Uhamiaji itahakikisha inakamilisha mahitaji ya waombaji wote waliotangulia ili iweza kurejesha utaratibu wa awali kupata pasipoti ndani ya siku saba.
Alisema kuwa waombaji wote waliocheleweshewa hati hizo watakuwa wamepata pasipoti zao ifikapo Aprili mwaka huu kwa kuwa mwishoni mwa mwezi huo, watakuwa wamerejesha utaratibu wa awali wa kupata hati hizo ndani ya siku saba.
0 Comments