Mgogoro huo ulianza mara baada ya wafugaji waliokuwa katika Bonde la Ihefu mkoani Mbeya kuhamishwa na Wilaya ya Rufiji ikafanywa kuwa moja ya maeneo ya kufikia wafugaji hao.
Mwezi Mei mwaka 2012 zilizuka vurugu katika Kata ya Ikwiriri wilayani humo zilizosababisha watu kujeruhiwa na mali kuharibiwa, ikiwa ni pamoja na kuvunjwa kwa nyumba za wafugaji baada ya mkulima mmoja wa Kijiji cha Muyuyu kudaiwa kuuawa na wafugaji.
Wakizungumzia vurugu hizo katika ziara iliyofanywa na Shirika la Kutetea Wafugaji wa Asili (Pingos Forum) wilayani humo hivi karibuni, baadhi ya wafugaji walimtuhumu Naibu Waziri wa Afya, Dk Seif Rashid wakisema kuwa hotuba zake ziliwahamasisha wakulima kuwashambulia.

“Vurugu zilianza baada ya baadhi ya wafugaji katika Kijiji cha Muyuyu kudaiwa kulisha kwenye shamba la mkulima ambaye baadaye alifariki dunia. Lakini mbunge alikuwa akihutubia mikutano na kuwaambia wakulima kuwa lazima watuondoe,” alisema Lago Laluka aliyevunjiwa nyumba.


Naye Abdallah Nyalando aliyevunjiwa kiwanda cha kusindika maziwa alisisitiza madai hayo: “Ninao ushahidi wa video zikimwonyesha mbunge wetu akiwahamasisha wakulima kuwaondoa wafugaji kwenye maeneo yao,” alisema Nyalando.

Hata hivyo, Naibu Waziri, Dk Seif Rashid amekanusha madai hayo akisema alikuwa akitekeleza uamuzi wa Baraza la Madiwani la wilaya hiyo.
“Unajua mtu anaweza kusema lolote, hata hapa tunapozungumza unaweza kuyatafsiri maneno yangu unavyotaka. Nilichokisema mimi ni kuhusu uamuzi wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Rufiji kwamba bonde hilo litumike kwa ajili ya kilimo siyo mifugo. Lengo ni kulitunza na uharibifu wa mazingira. Siyo Dk Seif kasema ni Halmashauri,” alisema Dk Rashid.

Dk Rashid ambaye ni mbunge wa Rufiji amesisitiza kuwa eneo hilo siyo la wafugaji.

“Hilo tatizo liko nchi nzima na hata kabla sijawa mbunge nililifahamu na nilipokwenda Bungeni nilimuuliza Waziri wa Mifugo akanijibu kuwa eneo hilo siyo la wafugaji bali ni la kilimo tu,” alisema.

Akizungumzia uamuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza aliyeagiza kuwa wafugaji hao wasiondolewe hadi watakapopatiwa maeneo mengine, alisema kauli hiyo si lolote kama haifuati sheria ya mwaka 1975.
“Agizo la mkuu wa mkoa linapaswa kwenda na sheria ya mwaka 1975 inayotaka bonde hilo liwe la kilimo na waziri alishajibu hivyo,” alisisitiza Dk Rashid.

Dk Rashid amedaiwa kutoa kauli za kuwachochea wakulima kuwaondoa wafugaji hao kwa madai ya kuingilia mashamba ya wakulima siku chache kabla ya kutokea kwa vurugu hizo.
Baadhi ya wakulima wa Ikwiriri wilayani humo wameilaumu Serikali kwa kutowaelekeza wakulima kwenye maeneo waliyopangiwa.
“Serikali ndiyo imewaelekeza wakulima kuja hapa Rufiji na kila siku wanachukua fedha za vibali, lakini wameshindwa kuwapeleka kwenye maeneo yao,” alisema Juma Ngwele. Naye Mwajuma Mwinyikambi aliwalaumu wafugaji kwa kulisha mifugo yao kwenye mashamba ya watu.

“Tangu wamekuja hao wafugaji hapa amani imepotea kabisa, kwa kweli hatuwataki. Ni kweli tunapata maziwa na nyama kwa urahisi, lakini ni wakorofi, wanaharibu mazao yetu kila mara,” alilalamika Mwajuma.
Kauli ya mkuu wa mkoa
Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza alisema agizo lake lilikuwa ni wakulima kwenda kwenye maeneo waliyopangiwa na siyo vinginevyo.

“Agizo langu lilikuwa ni la mpango kazi. Mwaka 2008 wakati Serikali inawahamisha wafugaji kutoka Bonde la Ihefu, Wilaya ya Rufiji ilikuwa ni moja ya maeneo waliyotakiwa kufikia. Nilichoagiza ni wakulima kwenda kwenye maeneo waliyopangiwa, siyo vinginevyo,” alisema Mahiza na kuongeza:
“Wafugaji waliokwenda kwenye maeneo yao waliyopangiwa, tumewaacha, ila wale walio kwenye maeneo yasiyoruhusiwa waondoke.”
Serikali haikujiandaa?
Akizungumzia kero za wafugaji wilayani humo, Ofisa Ardhi, Maliasili na Mazingira, Leo Rwegasira amekiri kwamba Serikali haikuwa imeandaa maeneo ya kuwaweka wafugaji baada ya kuhamishwa kutoka Bonde la Ihefu.Kabla ya kuja kwa wafugaji hawa hapa Rufiji palikuwa shwari, lakini walipokuja mwaka 2007 imekuwa ni vurugu tupu. Awali tuliambiwa kuwa kuna mifugo itakayobaki hapa, mingine itakwenda Lindi na Mtwara hivyo maeneo yaandaliwe. Lakini hadi wanafika hakukuwa na maeneo ya kuwaweka na hakukuwa na fedha za kuainisha maeneo hayo,” alisema Rwegasira.
Kutokana na hali hiyo, alisema kuwa walitenga vijiji tisa ambavyo waliainisha maeneo ya wafugaji harakaharaka. Akizungumzia uwezo wa eneo hilo kuchukua mifugo, alisema kuna hekta 7874 zenye uwezo wa kuchukua mifugo 39,362, lakini hadi sasa kuna mifugo 109,239.
Akizungumzia Kampuni ya Mkiu Poultry farm iliyopewa eneo la uwekezaji badala ya wafugaji wa ng’ombe, Rwegasira alisema huo ulikuwa ni uamuzi wa vijiji hivyo na walipata kibali cha kamishna wa ardhi.
Hata hivyo, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk David Mathayo amekanusha kuwa Serikali ilikurupuka kuwahamisha wafugaji hao.
Dk Mathayo amekwenda mbali zaidi na kusema kuwa Tume ya matumizi bora ya ardhi inayoshirikisha Wizara za Maliasili na Utalii, Mifugo na uvuvi na Wizara ya Ardhi inaendelea na upimaji wa maeneo ya wafugaji wanaohamishwa.

Rushwa yatawala
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili wilayani humo umebainisha kuwa Serikali haikuwa imetayarisha eneo maalumu la kuwahamishia wafugaji hao,hali inayowafanya wasumbuliwe na viongozi wa vijiji wanaowadai fedha ili wawape waeneo ya kulisha mifugo hiyo. Mmoja wa wafugaji hao kutoka Kijiji cha Muyuyu, Mbuga Pawa alisema kuwa tangu walipofika wilayani humo wamekuwa wakilipia fedha za usajili kila unapokuja uongozi mpya.“Mara ya kwanza tulipokuja tulilipia vibali vya kukaa katika vijiji kwa Sh30,000, baadaye tukaambiwa siyo halali, tukasajiliwa tena kwa vibali vingine kwa Sh80,000 na wengine sasa wanasajiliwa kwa Sh100,000. Hadi sasa hatujui hasa ada ya kusajiliwa ili tupewe maeneo ni shilingi ngapi,” alisema Pawa.
Wafugaji wengine wa jamii ya Mang’ati, Saleh Chafuchafu, Masharubu Chafuchafu na Masauda Chafuchafu wanalalamika kufukuzwa katika vijiji vya Kilimani A na B licha ya kuishi tangu mwaka 2006.
Akizungumzia tuhuma hizo, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ngorongoro, Uwesu Mbembeni amekiri kuwepo kwa vitendo vya rushwa huku akimtaja aliyekuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngorongo Magharibi, Hassan Mpange kuwa alikusanya kiasi cha Sh665,000 kwa wafugaji akidai ni ada ya kuwajadili ili waruhusiwe kuishi na mifugo yao. Juhudi za kumpata Hassan Mpange kujibu tuhuma hizo hazikufanikiwa kutokana na kukata simu kila anapopigiwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngorongo Magharibi, Mohamed Mkwega amekiri kuchukua fedha za wafugaji hao akidai ni ada ya uvamizi na posho za kikao.
Naye Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Juma Kilalile alisema tatizo la wafugaji katika vijiji hivyo kuzidiwa na idadi ya mifugo.

Takukuru Rufiji
Akizungumzia malalamiko hayo ya rushwa, Ofisa wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) wilayani Rufiji, Saada Mzimba amekiri kuyapata malalamiko ya rushwa kutoka kwa wafugaji na kwamba tayari kuna kesi mbili baada ya malalamikio hayo.
“Ni kweli tunapata malalamiko hayo, kwa mfano kuna wafugaji kutoka Kijiji cha Mkongo walifika hapa kulalamika. Huwa tunauliza kama wamepata vibali vya kuishi vijiji hivyo, maana wengine wanavamia tu,” alisema na kuongeza:“Hadi sasa tuna kesi mbili tumewafungulia viongozi wa vijiji wanaodai rushwa. Vilevile tunawashauri waende kwenye maeneo waliyoandaliwa badala ya kutangatanga.”