Viongozi wa Taifa wakishangilia jambo siku ya kuazimisha kwa miaka 49 ya Muungano wa Tanzania, sherehe zilizofanyika katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam 

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni muungano wa mfano duniani. Ni dola mbili huru zilizoungana na kuunda nchi moja yenye serikali mbili.

Tanganyika ilipata uhuru wake Desemba 9/1961 na ikapata kiti chake katika Umoja wa Mataifa Desemba 14, 1961. Namba ya kiti hicho ni ‘GA resolution 1667 (XVI).’ Zanzibar nayo ikapata uhuru wake Desemba 10, 1963 na ikapata kiti chake katika Umoja wa Mataifa Desemba 16, 1963; namba ya kiti hicho ni ‘GA resolution 1975 (XIII).’

Ilipofika Aprili 26, 1964, mataifa hayo mawili huru yaliungana na hapo ndipo ilipozaliwa nchi iliyojulikana kwa jina la Tanzania.
Novemba 2, 1964 kupitia Wizara wa Mambo ya Nchi za Nje ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliuandikia barua Umoja wa Mataifa na kutaka Zanzibar na Tanganyika ziondoshwe katika orodha ya mataifa na iingizwe nchi inayojulikana kwa jina la Tanzania.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni sawa na muungano wa Siria na Misri walioungana mwaka 1958 na ni sawa na muungano wa Yemen ya Kaskazini na Yemen ya Kusini walioungana mwaka 1990. Kwa bahati mbaya muungano wa Siria na Misri ulivunjwa mwaka 1961 (ulidumu kwa miaka 3).

Kwa sasa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umefikia hatua nzuri na ya kupigiwa mfano duniani kwa sababu umedumu kwa miaka 49 sasa.
Hata hivyo pamoja na kuwa muungano huu una muundo wa kipekee na kuwa umedumu kuliko miungano mingi iliyowahi kuwapo Afrika.

Muungano wa kwanza ulikuwa ni ule wa nchi za Afrika Magharibi, mwishoni mwa miaka ya 50 na mwanzoni mwa miaka ya 60, ulioanza na nchi mbili Ghana na Guinea na baadaye Mali ikajiunga nao. Muungano huu ulitokana na vuguvugu la umajimui wa Afrika (Pan Africanism), vinara wake wakiwa Kwame Nkrumah wa Ghana, Sekou Toure wa Guinea na Modibo Keita wa Mali.

Novemba 1958 uliundwa muungano wa Ghana na Guinea mara baada ya mkutano wa watu wa Afrika (All- African Peoples’ Conference). Ghana ilitoa fedha nyingi na kuipa Guinea ili ijitoe haraka kutoka katika utegemezi wa Ufaransa.

Mei 1959 ikatangazwa kuwa umoja huo utatambulika kama Umoja wa Dola za Kiafrika.

Ilipofika Aprili 1961, Mali nayo ilijiunga na umoja huo. Muungano huo ulivunjika mwaka 1962 kutokana na vita baridi, ambapo Guinea ilionekana ikiinyooshea mikono Marekani wakati wenzake walikuwa wakifuata mrengo wa kushoto wa Karl Marx/Lenin
Muungano mwingine wa nchi za Afrika ulifanyika mwaka 1981 baina ya nchi za Senegal na Gambia, uliojulikana kama Senegambia ambao ulikufa mwaka 1989.

Pamoja na kuwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni muungano wa kupigiwa mfano, lakini bado si vyema kuacha kusema kuwa una matatizo.