Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene 
Dodoma.
 Wizara ya Nishati na Madini imerudia kauli yake kuwa itashusha umeme kwa kila kijiji kitakachokuwa kimepitiwa na umeme wa gridi ya Taifa bila ya kuruka.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Ferister Bura (CCM)ambaye alitaka kujua ni lini umeme utapelekwa katika Kijiji cha Chipogoro katika Wilaya ya Mpwapwa.

Mbunge huyo alihoji kuwa ahadi ya kupeleka umeme katika kijiji hicho ni ya Serikali ambayo ilitolewa na makamu wa rais alipofanya mkutano katika eneo hilo hivyo akataka kujua ni lini umeme utashuka hapo.
Awali katika swali la msingi, Ahmed Shabiby (Gairo-CCM) alitaka kujua utekelezaji wa kupeleka umeme katika vijiji vya Chakwale na Rubeho utakamilika lini pamoja na miradi ya umeme ya REA katika vijiji vya Chakwale-Madege, Idibo, Iyogwe na Kikunde.Simbachawene alisema utekelezaji wa kupeleka umeme katika kijiji cha Chakwale na Rubeho ni kazi ya nyongeza katika awamu ya kwanza ya miradi ya umeme vijijini Mkoa wa Morogoro.
Alisema kuwa mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi aitwaye Symbion Power LLC na unahusisha ujenzi wa njia ya kusambaza umeme ya Msongo Kv 33 na umbali wa Kilomita 22.
Kuhusu Vijiji vya Gairo alivitaja Mswaki, Mgera, Kwamaligwa, Mtumbatu, Madege, Idibo, Iyogwe na Kikundi ambavyo kazi ya kupeleka umeme katika maeneo hayo iko katika hatua nzuri.
Mwisho.