Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia (WB) nchini, Philippe Dongier akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana baada ya mkutano wa kujadili hali ya ukuaji uchumi  wa Tanzania, kama itainua uchumi wake kwa kufanya maboresho sekta za bandari. Picha na Venance Nestory 

Dar es Salaam.
 Bandari ya Dar es Salaam imekuwa ikilikosesha taifa Dola 1.8 bilioni za Marekani (Sh2.8 trilioni) kwa mwaka, kutokana na kukosa ubora wa biashara.

Kutokana na hali hiyo, wataalamu wameeleza kuwa bandari hiyo inahitaji kufanyiwa maboresho muhimu ya hali ya juu, ili fedha hizo zisaidie nchi kuacha kutegemea misaada ya maendeleo.

Kwa mujibu wa ripoti iliyopo kwenye kitabu cha Opening the Gates: How the port of Dar es Salaam can transform Tanzania, licha ya Bandari ya Dar es Salaam kuwa sehemu nzuri, imekosa uwezo hivyo usimamiaji sera bora za kuiboresha zinatekelezwa taratibu. Ripoti hiyo inaeleza kuwa, mwaka 2012 pekee bandari hiyo ilikosesha taifa kiasi hicho cha fedha, huku ikizikosesha nchi jirani Sh1.3 trilioni.
“Fedha hizo ni sawa na asilimia saba ya pato la taifa, kitu ambacho kinawaathiri wanunuzi, wafanyabiashara na wakala mbalimbali wa Serikali,” inaeleza.

Mchumi Mkuu wa Benki ya Dunia (WB), Jacques Morisset ameihimiza Tanzania kuifanya bandari hiyo kuwa moja ya vipaumbele vyake vya juu kwa ajili ya kukua kwa uchumi.

“Watumiaji Bandari ya Dar es Salaam wanalipa fedha nyingi kwa wasimamizi wa bandari na wakala mbalimbali, kwa ajili ya huduma zao kuliko Mombasa,” alisema Morisset.Akizungumzia ripoti hiyo, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alisema Serikali imekuwa ikijitahidi kuboresha bandari hiyo, lakini kazi ya ziada inahitajika kuifanya iweze kushindana na nyingine. “Tunahitaji nchi jirani ziendelee kuitumia bandari yetu, bado tuna kazi kubwa ya kufanya ndiyo maana niko hapa, tunahitaji kuimarisha Kitengo cha Operesheni na maeneo mengine,” alisema Dk Mwakyembe.