Dar es Salaam.
Hatimaye hali ya afya ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Nchini, Robert Manumba, imeimarika na amerejea kazini.
Akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso, alikiri kuwa Manumba amereje kazi ingawa hakuwa tayari kutaja tarehe aliyoingia kazini.
“ Eh! Unauliza nini, mbona ameanza kazi siku nyingi, siwezi kukumbuka tarehe sipo ofisini naelekea kwenye kikao cha kazi,” alisema Senso.
Habari za kuaminika kutoka kwa baadhi ya maofisa wa kitengo cha upelelezi, zilisema kiongozi huyo ameshaanza kazi baada ya afya yake kutengemaa.
Mwandishi wa habari hizi, aliwasiliana na Manumba ambaye kwa kifupi alisema “Kwa sasa sijambo, ninakwenda kwenye mkutano.” Mkurugenzi huyo alirejea nchini April 22, mwaka huu akitokea Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa katika Hospitali ya Millpark.
Amekuwa katika hospitali hiyo kwa zaidi ya miezi miwili, kuanzia Januari 26, mwaka huu akisumbuliwa na malaria.
Hatua ya kumpeleka Afrika Kusini, ilikuja baada ya kulazwa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi katika Hospitali ya Aga Khan Januari 13, mwaka huu, akiwa hajitambui,.Alikuwa akipumua kwa msaada wa mashine.
na viongozi mbalimbali wakiwamo wa Serikali walikwenda kumjulia hali.
Manumba amerejea baada ya madaktari waliokuwa wakimtibu kujiridhisha juu ya kuimarika kwa afya yake.
|
0 Comments