Raia wa Iran Ahmad Mohammed na Sayed Mousavi wamefungwa maisha
Raia wawili wa Iran wamehukumiwa kifungo cha maisha katika mahakama moja ya
Kenya kuhusiana na mashtaka ya ugaidi.
Raia hao ni Ahmad Mohammed na Sayed Mousavi ambao walishtakiwa wiki iliyopita
kwa kumiliki vilipuzi, ambavyo inaaminika vilikuwa vitumiwe kwa kufanya
mashambulizi.
"mwili unanisisimka nikifikiria hasara ambayo ingesababishwa na shambulizi
hilo la kigaidi," amesema jaji Kiarie Waweru Kiarie, kama linavyoripoti shirika
la habari la AFP.
Hata hivyo, serikali ya Iran imekana kuhusika na mpango huyo wa kuishambulia
nchi ya Kenya.
Siku ya Jumapili, balozi wa Iran nchini Kenya, Malik Hussein Givzad, amesema
ubalozi utasaidia familia za washtakiwa hao kukata rufaa dhidi ya hukumu
iliyotolewa.
"kama ubalozi, tunachoweza kufanya ni kuzisaidia familia za washtakiwa kukata
rufaa, iwapo mawakili wanahisi kwamba hakuna ushahidi wa kutosha," amenukuliwa
balozi Givzad na gazeti la Kenya Daily Nation.
"nchi ya Iran ina uhusiano mzuri wa kibiashara na Kenya. Huu ulikuwa ni
mchakato wa kisheria, tunauheshimu." ameongeza kusema.
Mahakama ilibaini kwamba Mohammed na Mousavi ambao wanahusishwa na mtandao
ambao unapanga njama ya kulipua mji wa Nairobi na sehemu ya pwani ya nchi hiyo
Mombasa.
Jaji Kiarie amesema ameamua kuwafunga maisha kwa sababu ya vilio vya
waathirika wa milipuko iliyopita vilisikika zaidi kuliko kujitetea kwao,
imeripoti AFP.
Mawakili kutoka upande wa utetezi wanadai kwamba, Mohammed na Mousavi
walihojiwa na maafisa wa usalama wa Israel pindi walipokuwa wanashikiliwa.
Hata hivyo, upande wa mashtaka umekana tuhuma hizo. |
0 Comments