pembe za Ndovu zikiwa zimekamatwa

Arusha.
Kikosi kazi Maalumu cha Kupambana na Ujangili, kimemtia mbaroni mtu anayedaiwa kuwa kiongozi wa mtandao wa ujangili jijini Arusha aliyekuwa akisakwa kwa miezi miwili mfululizo.
Mtuhumiwa huyo anadaiwa kuwa ndiye anayepanga mipango yote ya ujangili katika hifadhi sita za wanyamapori zilizopo Kanda ya Kaskazini, kununua meno yote zya tembo na kutafuta masoko nje ya nchi.
Habari za uhakika zilizolifikia gazeti hili jana, zilisema kuwa mtuhumiwa huyo alitiwa mbaroni Jumatatu iliyopita eneo la Sakina jijini Arusha na kikosi kazi hicho cha kupambana na ujangili.
Kikosi kazi hicho kinaundwa na maofisa wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania(Tanapa), Kikosi cha Kupambana na Ujangili na Askari kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi (RCO) Mkoa wa Arusha.
Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa, Allan Kijazi, jana alilithibitishia Mwananchi Jumamosi kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo akimwelezea kuwa ni jangili hatari wa kimataifa, waliyekuwa wakimsaka kwa muda mrefu.

“Ni jangili hatari na sugu wa muda mrefu, ana mtandao mkubwa wa ujangili ndani na nje ya nchi na ndiye mnunuzi mkuu na mpangaji wa mipango yote ya ujangili,”alisema Kijazi.

Vyanzo huru vya habari ndani ya Jeshi la Polisi, vilieleza kuwa baadhi ya polisi wasio waaminifu walikuwa wakivujisha siri za mikakati ya kumkamata, hivyo kudhoofisha jitihada za kumnasa kinara huyo.
“Huyo jamaa ana pesa, kuna wenzetu walikuwa kwenye payroll (wanalipwa). Kwa hiyo mnaambiwa yuko hapa, mkienda mnakuta ametoroka, lakini walipogundulika ndiyo akakamatwa,”kilidokeza chanzo chetu.

Vyanzo hivyo  vimedai kuwa kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kunatokana na msukumo wa  tuhuma zilizoibuliwa bungeni na kambi rasmi ya upinzani Aprili 29 mwaka huu kwa Wizara ya Maliasili na Utalii na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.

Kwa mujibu wa mtoa habari wetu, baada ya kukamatwa, mtuhumiwa huyo alijaribu kuishawishi timu ya maofisa waliomkamata awape rushwa ya Sh10 milioni ili wamwachie, atoroke kwenda nje ya nchi.

Hata hivyo, kikosi kazi hicho, kilikataa kupokea rushwa hiyo na kumfikisha kituo cha polisi mtuhumiwa na sasa anashikiliwa Kituo Kikuu cha Polisi mjini Arusha akihojiwa.

Habari hizo zinadai kuwa mtuhumiwa huyo (jina tunalo) ndiye aliyefanikiwa kuwatoroka askari wa Tanapa Januari mwaka huu, walipolikamata gari la JWTZ likiwa na meno ya tembo.
Gari hilo aina ya Toyota Land cruiser VX lililokamatwa likiwa na namba bandia linadaiwa kuwa ni la Mwambata wa Kijeshi wa Zimbambwe hapa nchini na lilikamatwa eneo la Mto wa Mbu.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa, baada ya watuhumiwa ambao ni raia kukutwa na meno ya tembo katika tukio la kukamatwa kwa gari la JWTZ, walimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ndiye kiongozi wao.

Kijazi alifafanua kuwa kwa takriban miezi miwili walikuwa wakiweka mitego, lakini walishindwa kumnasa huku ikidaiwa kwamba mara kwa mara hubadili namba zake za simu za mkononi.

Alimpongeza RCO Arusha, kwa kufanikisha kazi ya kumkamata mtuhumiwa huyo sugu. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema hajapata taarifa akiahidi kufuatilia.Biashara ya meno ya tembo nchini imeonekana kushamiri siku hadi siku, ambapo mkoani Katavi Oktoba mwaka jana watu wawili mtu na mke wake walishikiliwa na polisi baada ya kukutwa na meno ya tembo yenye thamani ya Sh22 milioni