Mpenzi wa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa
Dar es Salaam.
Mpenzi wa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa, Josephine Mshumbusi ameshinda rufaa ya kupinga talaka yake, iliyofunguliwa na aliyekuwa mumewe wa ndoa, Aminiel Mahimbo.
Josephine kwa sasa amekuwa akiishi na Dk Slaa na tayari wamefanikiwa kupata mtoto mmoja, lakini harakati zao za kufunga ndoa zimekwama baada ya kupingwa na Mbunge wa Viti Maalumu wa Chadema, Rose Kamili akidai kuwa ana ndoa halali na Dk Slaa.
Mahimbo alikata rufaa hiyo katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, akipinga hukumu ya Mahakama ya Mwanzo Sinza iliyotoa talaka kwa Josephine dhidi yake, mwaka 2012.
Pamoja na mambo mengine, Mahimbo katika rufaa yake hiyo namba 32/2012, alikuwa akidai kuwa hapakuwa na ushahidi wa kutosha kiasi cha kuifanya Mahakama ya Mwanzo Sinza kutoa talaka hiyo.
Hata hivyo jana, Hakimu Aniseth Wambura aliyesikiliza rufaa hiyo, aliitupilia mbali ombi hilo akisema kuwa ameridhika na hukumu ya Mahakama ya Mwanzo Sinza kwamba kulikuwa na ushahidi wa kutosha kutoa talaka kwa Josephine.
Hakimu Wambura alisema katika hukumu hiyo,baada ya kupitia hoja za mrufani na za mjibu rufaa pamoja na mwenendo wa kesi ya msingi,amekubaliana na hukumu ya Mahakama ya Mwanzo Sinza kuwa ni sahihi.
Katika kesi ya msingi Josephine, alidai talaka kutoka kwa Mahimbo, pamoja na kudai kuwa Mahimbo hakuwa mwaminifu kwa kuwa alikuwa akitoka nje ya ndoa na kwamba alikuwa amemtelekeza bila kumpatia mahitaji na huduma za msingi, huku akimtesa.
Hakimu Wambura katika hukumu yake jana kwenye rufaa hiyo alisema, kutokana na sababu zilizotolewa na Josephine katika kesi ya msingi ni dhahiri kuwa hapakuwa na ndoa na kwamba mahakama haiwezi kuwalazimisha watu ambao hawapatani kuishi pamoja.
“Baada ya kusikiliza hoja za mrufani na mjibu rufaa ,mahakama hii imekubaliana hoja za mjibu rufaa (Josephine), kuwa kwa tabia ile mbaya na ukosefu wa uaminifu katika ndoa yake hapakuwapo na ndoa baina yao.”, alisema Hakimu Wambura.
“Hivyo mahakama hii inatangaza kuwa hukumu ya Mahakama ya Mwanzo Sinza ambayo iliivunja ndoa hiyo ilikuwa sahihi,” alisema kwa msisitizo Hakimu Wambura.
Wakili wa Josephine, Philemon Mutakyamilwa alisema kuwa amefurahishwa na hukumu hiyo akidai kuwa mahakama hiyo imetenda haki kwa mteja wake.
Licha ya kupangua kikwazo hicho, Josephine bado anakabiliwa na kikwazo kingine kilichomweka njia panda katika mipango yake ya kufunga ndoa na Dk Slaa.
Josephine na Dk Slaa walitarajia kufunga ndoa Julai 21, 2012, lakini imekwama baada ya Rose Kamili kufungua kesi Mahakama Kuu akiipinga kwa madai kuwa ana ndoa halali na Dk Slaa.
Pamoja na pingamizi hilo, Rose anamtaka Dk Slaa amlipe Sh50 milioni kama fidia ya kujihudumia pasipo matunzo ya mumewe huyo, huku pia akimtaka Josephine amlipe Sh500 milioni kama fidia ya maumivu aliyoyapata kutokana na kitendo chake cha kuingilia ndoa yake.
Kesi hiyo namba 4 ya mwaka 2012, inasikilizwa na Jaji Lawrance Kaduri, na itatajwa tena mahakamani hapo Julai 17, mwaka huu.
|
0 Comments