Rais Museveni anadaiwa kutaka mwanawe kumrithi kama Rais wa
Uganda anatakapoachia ngazi
Rais wa Uganda Yoweri Museveni amefanya mabadiliko katika
makamanda wake wakuu wa jeshi , huku kukiwa na taarifa za kutofautiana kwa
majenerali wa jeshi kuhusu ikiwa mwanawe Museveni anaweza kumrithi babake kama
rais.
Mkuu wa majeshi, Aronda Nyakairima aliyetajwa katika taarifa iliyofichuliwa
kuwa mmoja wa wanaopinga mwanawe Museveni Muhoozi Kainerugaba kumrithi babake,
amehamishwa hadi wadhifa wa kiraia kuwa waziri wa mambo ya ndani.
Taarifa za kutofautiana kwa majenerali jeshini ziliibuka mapema mwezi huu
wakati magazeti ya Uganda yalipochapisha barua kutoka kwa Generali mkuu David
Sejusa Tinyefuza, akidai kuwa Museveni anamtayarisha mwanawe kumrithi
atakapoachia ngazi.
Barua hiyo pia inasema kuwa Museveni anapanga kuwaua wale wanaopinga njama
yake.
Majenerali kadhaa wakuu walipinga barua ya Tinyefuza wakati kundi la wachache
likimuunga mkono.
Mabadiliko katika jeshi yanakuja baada ya magazeti makuu ya upinzani
yaliyotoa madai ya mgawanyiko jeshini , yakisalia kufungwa kwa siku ya tano huku
polisi wakiendelea kufanya msako katika ofisi zao kuitafuta barua hiyo.
Taarifa ya serikali imesema mabadiliko hayo sio makubwa bali ni madogo katika
kuhakikisha serikali inafanya vyema kazi yake.
Hata hivyo msemaji wa jeshi Paddy Ankunda alisema kuwa hayo ni mabadiliko ya
kawaida jeshini.
Ankunda alisema kuwa hakuna mgogoro jeshini na kuongeza kuwa Museveni ana
haki ya kufanya mabadiliko yoyote kama anavyoridhia.
Mkuu mpya wa majeshi ni Edward Katumba Wamala, ambaye amelimbikiziwa sifa
tele kwa kuongoza jeshi la Uganda katika vita dhidi ya wapiganaji wa kiisilamu
(Al Shabaab) nchini Somalia.
Ofisi za magazeti ya Daily Monitor na Red Pepper zilifungwa na kuzuiwa
kuchapisha magazeti yoyote na yameendelea kufungwa licha ya agizo la mahakama
kutaka polisi kuondoka katika ofisi hizo. |
1 Comments
Kama alivyowahi kusema mwalimu nyerere kadri kiongozi wa kiafrika anavyozeekea madarakani ndivyo anavyoshindwa kuachia madaraka. Msisahau huyu ni wa mbari ya kitutsi na alipata madaraka baada ya kuyapigania kwa kumwaga damu nyingi ya waganda. Anaona ni bora warithi mwanaye na mkewe kuliko kuwaachia waganda wengine uongozi.