Watu walipomwona ndipo wakamzunguka na kuanza kuimba nyimbo za kumsifu na kumshangilia: “Rais wetu... Rais wetu... Rais wetu.”
Maofisa wa Polisi walimfuata Mchungaji Msigwa na kumwomba aondoke lakini aligoma akidai ni mwakilishi halali wa wananchi kwa hiyo hawezi kuondoka.
Badala yake alipanda kwenye gari lake na kuanza kuzunguka eneo hilo huku akifuatwa na umati wa watu. Polisi nao walikuwa wakimfuatilia kwa magari yao.
Baada ya idadi ya watu kuongezeka kwa wingi barabarani na kuanza kufanya kitu kama maandamano wakiwa nyuma ya gari ya Msigwa, polisi waliwataka kutawanyika lakini waligoma huku wakizidi kuimba nyimbo za kumsifia mbunge huyo.
Mabomu ya machozi
Ilipotimu saa tatu na nusu asubuhi, polisi walianza kutumia magari ya kumwaga maji ya kuwasha na kutumia mabomu ya machozi na kusababisha watu kukimbia ovyo, huku wengine wakikusanya mbao, matairi na mawe na kuwasha moto ili kuwazuia polisi wasiwafikie.
Moto huo ulisababisha nyumba moja kuwaka moto ndipo gari la zimamoto lilipokwenda kuzima lakini nalo likashambuliwa.
Msigwa kukamatwa
Mchungaji Msigwa alikamatwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Kabla ya kukamatwa, aliwaambia waandishi kuwa polisi walikuwa wanawaonea wafanyabiashara hao na kwamba manispaa haikuwa na mamlaka ya kisheria ya kuwazuia wafanyabiashara hao.
Mei 15 na 16, mwaka huu Msigwa alifanya mikutano ya hadhara kwenye Viwanja vya Mwembetogwa na Magorofani na kuwataka wafanyabiashara kutokuogopa kufanya shughuli zao kwenye eneo la Mashine Tatu.
0 Comments