TUME ya kuchunguza sababu za kufeli
kwa kiasi kikubwa kwa wanafunzi wa kidato cha nne waliofanya mitihani ya
kuhitimu mwaka 2012 imekamilisha kazi yake na taarifa za uhakika
zilizolifia gazeti hili zinasema , upangaji alama zao utafanyika upya.
Kama ambavyo gazeti hili lilivyobaini
katika uchunguzi wake wa kiuandishi kwamba kulifanyika mabadiliko ya
utoaji alama kwa ajili ya mitihani waliyofanya wanafunzi mwaka huo
(2012) bila maandalizi kwa wadau, tume hiyo imependekeza alama zipitiwe
upya (regrading).Katika alama za awali, alama D anapoyopewa mtahiniwa
baada ya mtihani wake kusahihishwa ilikuwa ni kuanzia alama 21 kwenda
mbele na F ilikuwa 20 kushuka chini lakini katika mabadiliko yaliyoleta
‘maafa’ ya kufeli kwa watahiniwa wa mwaka jana, alama D ilianzia 35 na
kuendelea, wakati ile ya kufeli (F) ilianzia alama 34 kushuka chini.
Vyanzo mbalimbali vya habari
vimeeleza ya kwamba Jumatatu wiki hii, Baraza la Mawaziri lilikutana
mjini Dodoma na kujadili, pamoja na mambo mengine, uamuzi wa kurejea
upangaji alama za mitihani hiyo ya wanafunzi iliyosahihiswa kwa kutumia
alama za juu (yaani kufeli ni kuanzia alama 34 badala ya 20).
“Baraza limeafikiana na ripoti kwamba
upangaji alama ufanyike kwa vigezo vya zamani kwa sababu uamuzi wa
kutumia alama mpya ulifanyika bila maandalizi ya kutosha, ikiwa ni
pamoja na kutowapa muda wa kutosha wadau.
“Mitihani ya shule na kikanda ilikuwa
ikiandaliwa na kusahihishwa kwa alama za zamani, kumbe kulikuwa na
alama mpya zimewekwa kitaifa, kwa hiyo kuna uzembe ulifanyika wa
kuwafahamisha wadau kwa wakati,” kinaeleza chanzo kimoja cha habari.
Katika uchunguzi wake, Raia Mwema
lilibaini kasoro kadhaa zilizochangia kufeli kwa idadi kubwa ya
wanafunzi katika mitihani ya kidato cha nne mwaka 2012 na kati ya kasoro
hizo ni kutumia alama mpya za kupanga matokeo badala ya alama za
zamani, bila kufanyika kwa maandalizi ya kutosha.
Kutokana na kufeli huko, Februari
mwaka huu, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliunda tume ili kuchunguza sababu
za kufeli kwa wanafunzi wengi waliohitimu kidato cha nne mwaka 2012.
Katika matokeo hayo ya kidato cha nne 2012, asilimia 60 ya wanafunzi
waliofanya mtihani wa kuhitimu walipata daraja sifuri.
Tume hiyo ilihusisha baadhi ya wadau
wakiwamo kutoka shule na vyuo binafsi vya elimu, Kamati ya Bunge ya
Huduma za Jamii na Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania
(Tahossa), asasi zisizo za kiserikali (NGOs) zinazojishughulisha na
masuala ya elimu.
0 Comments