Na Mwandishi Wetu
TAKRIBAN mwaka mmoja tangu alipoeleza aina ya jeneza atakalotaka azikwe siku akifa, mwanamuziki Judith Wambura 'Jide' au 'Anaconda' ameibua jingine jipya, safari hii ameandika wosia wa kifo chake, Ijumaa lina uchambuzi kamili.ATIMIZA AHADI Kama alivyoahidi mashabiki wake wiki moja iliyopita kupitia mtandao wake wa kijamii, Jumatano ya Mei Mosi, mwaka huu, mishale ya saa 8:00 mchana, Jide au Komando aliandika wosia huo wenye maneno 555 akiwataja watu ambao asingetaka wafike kwenye msiba wake siku akifariki dunia.
NI KWA WATANZANIA WOTE Katika sentensi nyingine, mwanadada huyo ameandika wosia huo kwa Watanzania wote watakaokuwa bado hawajatangulia mbele ya haki yeye atakapofikwa na mauti.
ASIOTAKA WAFIKE Katika wosia huo, Jide alitupa tuhuma nzito kwa mabosi wa Clouds Media Group hasa Radio Clouds FM, Joseph Kusaga na Ruge Mutahaba kuhusika katika kumhujumu kwenye tasnia ya muziki nchini huku akiwataka wasifike kuaga maiti yake.
RADIO ISITANGAZE KIFO CHAKE Katika kuupitia wosia huo, Ijumaa limebaini kuwa, Jide alizuia Kituo cha Radio Clouds FM kisitangaze kifo chake wala kupiga nyimbo zake siku atakapokufa.
AJITOA FIESTA, KISA? Ndani ya wosia huo, mwanamuziki huyo aliendelea kudai kuwa alijitoa kwenye shoo za Fiesta zinazofanyika kila mwaka ambapo kwa mara ya mwisho alilipwa Sh. 800,000 na kuanzia hapo ndipo fukuto la kubaniwa lilipoanza. Alisema bifu likapamba moto mwaka 2003 alipotoa albamu yake ya pili iliyojulikana kwa jina la Binti.
KISA? MACHOZI BAND Aliandika kuwa tatizo lingine lililochochea yeye kukandamizwa ni baada ya kuacha kufanya shoo za Clouds na kuanzisha bendi yake ya Machozi ambapo alijiajiri mwenyewe na kupata mafanikio jambo ambalo anadai jamaa hao hawakulipenda hivyo kuanza kuchochea mbinu za ‘kumuua’ kisanii.
KUKANDAMIZWA Aliwatuhumu kuwa kwa muda mrefu ‘wabaya’ wake hao wamekuwa wakifanya njama za kumkandamiza ili kuhakikisha anapotea kabisa kwenye muziki.
ASISHIRIKIANE NA WASANII WENGINE? Alizidi kuandika kwamba watu hao wamekuwa wakitishia kutopiga nyimbo zake alizoshirikishwa na wasanii wengine wa Bongo.
FITINA Jide aliandika: Nilinyamaza kwa muda mrefu lakini kadIri muda ulivyosonga mbele ndivyo hali ilivyozidi kuwa mbaya kwani jamaa hao waliongeza fitina kwangu kila kukicha.
VIKAO VINNE Jide aliendelea kutuhumu kuwa jamaa hao hadi sasa walishakaa vikao vinne vilivyolenga kumpoteza kabisa kwenye ramani ya muziki huku akidai ni wafitini ambao wamekuwa wakipita kila mahali kuhakikisha wanaziba mrija wa kumuingizia ‘chochote kitu’.
UPANDE WA PILI UNASEMAJE? Baada ya kuutathimini wosia huo na kuona ni kwa jinsi gani ulivyojaa tuhuma zilizohitaji majibu, kama kawaida ya Ijumaa lililojaa weledi lilitafuta upande wa pili, Clouds Media Group ili kupata majibu ya kile alichokiandika msanii huyo. Mmoja wa mabosi wa Clouds ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa kuwa si msemaji wa kampuni, pamoja na kukiri kuuona wosia huo, alichambua kipengele kimoja baada ya kingine.
KUHUSU KUBANIWA “Kama ana ushahidi ni lini alibaniwa aweke data mezani. Unajua watu wametengeneza kizazi cha chuki bila kuwa na sababu ya msingi. “Hata msanii chipukizi akiibuka leo ataambiwa fulani anabaniwa na kujikuta akijenga chuki bila kujua anayeeneza hayo ana lengo gani. “Ipo mifano ya wasanii wengi ambao nyimbo zao hazipigwi katika vituo f’lanif’lani vya redio (akavitaja) kama Diamond na Juma Nature, mbona huko hawapaoni wanaona Clouds pekee?”
KUHUSU KUKANDAMIZWA “Kama kuna ushahidi ni lini aliandaa shoo au aliitwa kwenye shoo then (halafu) watu wakamkandamiza kwenye malipo auweke wazi, kwani hakuna mikataba? Ingekuwa ni vizuri akatoa mikataba kuwa alikandamizwa kuliko kujenga chuki zisizokuwa na msingi. Anasema alilipwa shilingi laki nane, kwa nini hakukataa? Kwani alilazimishwa?”
KUHUSU ASISHIRIKIANE NA WENZAKE “Ukweli ni kwamba hatujawahi kubana kupiga wimbo wa mtu kisa ameshirikishwa yeye. Hayo ni maneno ambayo mwisho wa siku hawezi kuthibitisha kwa data.”
KUHUSU KUMFITINI “Mtu amfitini ili apate faida gani? Kama hakuna faida hakuna sababu ya kumfitini mtu katika biashara yake.”
VIKAO VINNE NA KIFO “Hayo mengine ya vikao mimi siyajui na siwezi kuzungumzia kifo cha mtu kwani huo ni wosia wake.”
KUNA KITU KIKUBWA KINAKUJA Kwa mujibu wa bosi huyo, hali inavyoendelea kuna kitu kikubwa kinakuja na ili kuweka sawa mambo haya, Clouds wataitisha mkutano mkubwa wa waandishi wa habari ili kuifahamisha jamii ni nini hasa kinaendelea. Baada ya bosi huyo kutoa ufafanuzi juu ya tuhuma za msanii huyo, Ijumaa lilimtafuta meneja wake Jide, Gardner G. Habash ili aweke wazi kama tuhuma alizotoa mwanamuziki huyo zina ushahidi wa kushika, lakini bila mafanikio.
JIDE KATIKA SIKU ZA KARIBUNI Katika siku za hivi karibuni, Jide amekuwa akitumia mitandao ya kijamii kueleza jinsi anavyoandamwa na kituo hicho cha redio na kusababisha kuibuka kwa mijadala mbalimbali kutoka kwa wasomaji wake.
|
0 Comments