Dodoma.
Rais Jakaya Kikwete ameshauriwa kuondoa kigugumizi na masuala ya kulindana, ili kuinusuru nchi ya Tanzania isitumbukie katika shimo refu zaidi la umasikini kuliko ilivyo sasa.
Wito huo ulitolewa jana na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Tawi la Afrika Kusini na nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, Kelvin Agutu Nyamori, alipozungumza na gazeti hili nje ya viwanja vya bunge mjini Dodoma.
Nyamori alibainisha kuwa kinachoiua Tanzania ni kitendo cha kuoneana haya ndani ya CCM na Serikalini ambako kunafanywa na viongozi wa juu akiwemo Rais Jakaya Kikwete.
“Nikisema rais ana kigugumizi na amekuwa akiwaonea haya zaidi watu sio kwamba namkashifu wala si kwamba nimemdharau, bali nataka atimize wajibu wake kwa kuwawajibisha wabovu na wazembe na kuwapa nafasi wachapa kazi kusonga mbele,” alisema Nyamori.
Alisema ukimya wa rais unafanya wananchi waamini na ndivyo ilivyo kwamba hakuna kiongozi mzuri atakayekuja kupatikana kutokana na wengi kuendelea kurithishana nafasi za uongozi kwa hofu ya kulinda vitumbua vyao,lakini bado kiongozi mkuu anashindwa kuwawajibisha wenye mitazamo hiyo.
Mwenyekiti huyo aliwatupia lawama washauri wa Rais Ikulu,kwamba wameshindwa kutimiza wajibu wao kiasi cha kumfanya aonekane kama hafai kwa jamii anayoiongoza.
Akizungumzia msimamo wa CCM kwa sasa, alisema chama hicho kikongwe kimepoteza mwelekeo kwa kiasi kikubwa na kimegawanyika kutokana na maslahi na matakwa ya wanasiasa ambao wengi sio wema.
“Tuna vyama vya CCM viwili kwa sasa, kimoja ni CCM ya Mwalimu Nyerere ambayo ni CCM nambari One, na ya pili ni CCM ya mabepari na mabeberu ambayo haijui kama kuna watu wa kada ya chini na badala yake wao wanajipendelea wenyewe,” alisema.
Alishauri kuwepo na mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwa Watanzania bila ya kujali itikadi zao za vyama vya kisiasa kwani Tanzania kwanza mambo mengine nyuma.
----------------------------
Mwananchi.
|
0 Comments