Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia, wakifanya doria katika moja ya maeneo ya Mji wa Mtwara. 

Chanzo cha vurugu kuhusu gesi zilizotokea hivi karibuni mkoani Mtwara, kinaelezwa kuwa ni vuguvugu la kisiasa lililowaingia wananchi kiasi cha kujenga chuki kubwa dhidi ya Serikali baada ya kupata mahubiri ya wanasiasa.
Inaelezwa kuwa mzozo huo ulianza rasmi mwaka jana baada ya Serikali kuituma kamati ya kuratibu Maoni ya Sera ya Gesi ambayo ilifika mkoani Mtwara, Novemba 16, mwaka jana kukusanya maoni ya wananchi.

Katika mikutano yake mjini Mtwara, inaelezwa kuwa wananchi wengi hawakukubaliana na wazo la kusafirisha gesi kwenda nje ya Mtwara kwa njia ya bomba.

Hali hiyo ndiyo iliyowafanya viongozi wa vyama vya NCCR-Mageuzi, TLP, UDP, ADC, DP, APPT Maendeleo, Sau na Chauma, kuungana na kuhamasisha wananchi kuhusu suala hilo.

Inaelezwa kuwa hilo lilifanyika Desemba 6, mwaka jana.
Katibu Mkuu wa Muungano huo, Selemani Litope ,alisema mikutano kati ya viongozi wa vyama hivyo na wananchi ilianza Desemba 12. Mikutano hiyo iliyopewa vibali na Jeshi la Polisi ilifanyika Desemba 12, 16, 19 na 22 na Desemba 27 yalifanyika maandamano makubwa.

“Tuliona kuna malalamiko mengi ya wananchi kuhusu suala gesi kusafirishwa kwenda Dar es Salaam, tukaona tuungane ili tufikishe kilio cha wananchi serikalini, kwa sababu tunaamini kwamba, kuisafirisha gesi hiyo ni kuwanyima wananchi fursa ya kufaidika,” alisema Litope.
Alisema katika maandamano yaliyofanyika Desemba 27, Litope alisema walimwandikia Mkuu wa Mkoa huo, Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia ombi la kutaka ayapokee lakini akakataa na kuwaita kuwa ni wapuuzi, jambo lililozidisha chuki ya wananchi.

“Kitendo cha mkuu wa mkoa kutuita wapuuzi ,kimeibua chuki kubwa miongoni mwa wananchi, hata hivyo maandamano yetu yalifanikiwa kwa sababu watu wengi walihudhuria na tukafanya mkutano katika Uwanja wa Mashujaa,” alisema.

Hata hivyo, Simbakalia alishaomba radhi kwa kauli yake hiyo Januari mwaka huu kupitia kikao cha majumuisho cha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Nani anayetuma vipeperushi na meseji?

Kabla ya vurugu zilizotokea Mei 22 mwaka huu, kulikuwa na vipeperushi na ujumbe wa simu uliosambazwa mjini Mtwara.
Moja ya waraka uliosambazwa Mei 17, ulisomeka: “Kusini zinduka, tuungane pamoja, maana dhamira ya Serikali haieleweki kwa mikoa ya kusini kama mnavyoona.Wote kwa pamoja saa 3.00 asubuhi ya Mei 17, 2013 tusikilize bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini bungeni, ili kujua mustakabali mzima wa gesi yetu na ili kuonyesha kilio/msimamo wetu kwa Serikali wa kutaka maendeleo kwa mikoa ya kusini.

Siku hiyo huduma zote za kijamii zisimamishwe ikiwa na maana ya maduka, masoko, daladala, pikipiki n.k ili iwe ujumbe kwa Serikali, maana JK ameamua kutumia nguvu nasi inabidi tupambane naye,” ulisomeka ujumbe huo.

Wakati Jeshi la Polisi likidai kuwakamata watu wawili wanaohusika kusambaza ujumbe wa simu, chanzo cha habari kimeeleza kuwa vipeperushi hivyo huchapishwa mjini Mtwara kwa siri kubwa.