INASIKITISHA na inauma, lakini ndiyo hali halisi, hatimaye mwili wa msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Albert Kenneth Mangweha, maarufu kwa jina la Mangwea, umezikwa jana kwenye makaburi ya Parokia ya Kihonda mkoani Morogoro ambapo ni jirani na nyumbani kwao marehemu.

Mwili wa Mangwea uliwasili mkoani hapo juzi baada ya msanii huyo kupatwa na umauti alipokuwa nchini Afrika Kusini, Mei 28, 2013, na kuzikwa kwenye makaburi hayo ambayo ni jirani na alipozikwa marehemu baba yake, Kenneth Mangweha miaka kadhaa iliyopita.
Umati wa watu uliojitokeza kuuaga mwili wa Mangwea, ulikuwa mkubwa ambapo wasanii mbalimbali, wanasiasa wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera na mbunge Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na wananchi wa kawaida, walijitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa Jamhuri ambako ndipo ulipoagwa kabla ya kwenda kuzikwa.

Kuwasili Morogoro
Wakati msafara uliobeba mwili wa Mangwea ukiwasili mkoani hapa jana jioni, umati ulikuwa mkubwa, watu walijipanga kwenye barabara, pikipiki zaidi ya 500 na magari mengi yote yaliungana kwenye msafara huo.
Msafara huo ulifikishwa nyumbani kwao na marehemu, baadaye kupelekwa hospitali kuhifadhiwa kabla ya kupelekwa kuagwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, jana asubuhi.

Uwanja wa Jamhuri watapika, geti lavunjwa
Hata kabla mwili haujafikishwa uwanjani hapo, idadi ya watu walioingia ilikuwa kubwa, lakini iliongezeka zaidi baada ya kuwasili.
Akitoa nasaha zake wakati akisoma risala uwanjani hapo, Sugu aliishauri serikali kuweka mkazo katika kuangalia haki za wasanii kwani idadi ya watu waliojitokeza kwenye msiba huo inaonyesha jinsi ambavyo sanaa yao inakubalika.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera ambaye alifika mpaka makaburini na kushuhudia mwili wa Ngwea ukifukiwa mchanga, naye aliwapa pole wadau wote wa tasnia ya muziki, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu na kusema kwa niaba ya serikali anatoa pole kwa wote na mipango ipo ya kuboresha kazi za wasanii.
Kutokana na idadi ya watu kuongezeka, ilifikia hatua askari wakazuia watu kuingia uwanjani hapo kwa kuwa walikuwa wamejaa ndani huku waliokuwa nje wakiwa ni zaidi ya wale waliokuwa ndani.
Wakati ulinzi ukiendelea, baadhi ya wananchi walivunja geti la kuingilia uwanjani hapo kutokana na kusukumana.
Kuona hivyo, ilibidi askari waongeze ulinzi ambapo askari wa kawaida waliongezeka wakajumuika na mabaunsa ndipo angalau mvutano ukatulia.
Watu hao waliovunja geti walikuwa wakitaka kuingia ndani ili kwenda kuuaga mwili wa Mangwea, lakini baada ya ulinzi kuongezeka, ndipo wakatulia na kuusubiri mwili utakapotoka wausindikize kwenda makaburini.

Watu wazimia, wajeruhiwa
Wakati hayo yakiendelea, ndani ya uwanja hali ilikuwa ya hisia sana ambapo watu sita walijeruhiwa kutokana na kusukumana, gazeti hili lilimshuhudia bibi mmoja akilia kwa maumivu kutokana na kusukumwa.
Lakini wakati huohuo wadada kadhaa walianguka na kupoteza fahamu wakati wakiwa ndani ya uwanja huo kulipokuwa kukifanyika shughuli ya kuuaga mwili.

Dully Sykes azuiwa kuingia uwanjani
Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Dully Sykes, alifika uwanjani hapo akiwa pamoja na rafiki zake, askari walimzuia kuingia uwanjani pamoja na gari lake lakini msanii huyo alikataa kuacha gari lake nje ya uwanja, ndipo yakazuka mabishano makali.
Lakini walinzi hao waliendelea kushikilia msimamo wao, ndipo Dully akakasirika na kuamua kugeuza gari akaondoka eneo hilo.

Familia yakana marehemu kuwa na mtoto
Akisimulia alivyopokea taarifa za msiba, mama mzazi wa Mangwea, Denisia Mangweha alisema:
“Kuna dada yake marehemu, anaitwa Magreth ndiye aliyeanza kupigiwa simu, ghafla akaitupa simu na kutoka nje, aliporejea ndani ndiyo akaniambia kilichotokea. Baadaye ndipo nikaanza kupigiwa simu kutoka sehemu mbalimbali.”
Alipoulizwa kuhusu taarifa za marehemu kuwa na mtoto, mama alisema: “Marehemu hajawahi kuniambia taarifa zozote kuhusu mtoto, ila najua tu kuwa kuna rafiki yake wa kike Mzungu ambaye ndiye aliyekuwa akija naye hapa

M to the P aibukia Jamhuri
Wakati umati wa watu ukiendelea na mchakato wa kuuaga mwili ndipo msanii, M to the P aliyekuwa na marehemu Afrika Kusini, alitokeza uwanjani hapo kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho kwa rafiki yake.
M to the P alilia sana mara baada ya kufika kwenye jeneza na kujikuta akiishiwa nguvu ambapo ilibidi apate msaada wa kushikiliwa na watu waliokuwepo eneo la tukio.
Baadaye wakati mwili ukiwa tayari umeshafukiwa, M to the P alizidiwa na kukimbizwa hospitali, ambapo hadi gazeti hili linaingia mitamboni haikujulikana nini kilichoendelea kutokana na msongamano uliokuwepo.

Mkoa wa Morogoro wazizima
Mara baada ya msafara wa kuubeba mwili kuutoa Uwanja wa Jamhuri kuupeleka makaburini ulipoanza, umati wa watu uliongezeka, wengi walijipanga barabarani na wengine kujiunga kwenye msafara huo.
Kila kona ambayo msafara huo ulipita, kulikuwa na watu wengi waliojipanga, hata walipofika makaburini idadi ya watu

Mtoto wa Mangwea aibuka
Wakati ndugu wakijiandaa kuusubiri mwili wa Mangwea makaburini, alijitokeza dada aliyejitambulisha kwa jina la Paulina Jeremiah na kusimulia kuwa yeye ni mama wa mtoto wa Mangwea.
Msanii wa filamu, Jack Wolper alijikuta akibebwa juujuu makaburini na baadhi ya vijana waliokuwepo eneo hilo kisha kumtupa kwenye shamba la mpunga, haikujulikana sababu ni nini hasa.
Vijana wengi pia walijitokeza wakiwa na mabango mbalimbali huku mara kadhaa wakiwashangilia mastaa waliokuwepo kwenye msiba huo.

Stori na Musa Mateja, Daudi Julian na Joan Lema kutoka Morogoro.
Akijielezea zaidi, Paulina aliyekuwa ameambatana na mtoto huyo, Neema Albert, alisema:
“Nilikutana na Mangwea wakati anasoma Mazengo, Dodoma na akanipa ujauzito, nikajifungua mtoto huyu (Neema), marehemu alimkubali na kusema kuwa kwa kuwa anasoma nimuache kwanza akimaliza tutafunga ndoa, nilimuelewa kwa kuwa ni kweli alikuwa akisoma.
“Baadaye aliwatuma ndugu zake kuja kwangu ambao ni Frank, Jotam na Aman ambao nao walikuja na kuniambia kuwa watafanya mpango pindi mambo yatakapokuwa tayari.
“Kwa sasa Neema anasoma darasa la pili katika Shule ya Iringa Mtumi, ipo Dodoma.”
Wakati Paulina akisimulia hayo, pembeni alikuwepo kaka mkubwa wa marehemu, Anton Kenneth Mangweha ambaye alikiri kuwafahamu watu hao na kusema ni sehemu ya ukoo wao. Anton akamchukua na kumuweka pembeni Paulina kisha kumwambia:
“Naomba ukae hapo pembeni tumalize kuzika kwa kuwa hili litakuwa jambo la kifamilia.”
Baadhi ya wasanii waliokuwepo eneo hilo, walianza kulia na wengine wakambeba mtoto Neema na kumpa pole Paulina.

Wolper atupwa shamba la mpunga