Mahakama mjini Cairo imewahukumu jela wafanyakazi 43 wa
mashirika ya misaada kwa kufanya kazi Misri kinyume na sheria.
Wafanyakazi hao walihukumiwa hadi miaka mitano gerezani baadhi hukumu ikitolewa huku wakiwa hawako mahakamani.
Pia iliamuru kufungwa kwa ofisi zao na kupigwa tanji kwa mali ya mashirika waliyokuwa wanafanyia kazi.
Kesi hiyo iliyoanza mwaka 2012 , imetatanisha uhusiano kati ya serikali ya Misri na Marekani.
Maafisa wa Marekani, wametishia kubana msaada kwa Misri ambao unatumia dola bilioni moja nukta tano pesa za msaada ambazo hutolewa kwa Misri kila mwaka.
Jumanne mahakama ya Misri iliwahukumu washukiwa 27 miaka mitano gerezani. Wengine watano walifungwa miaka miwili na wengine 11 walifungwa mwaka mmoja kila mmoja.
Washukiwa watano pekee wakiwemo raia mmoja mmarekani walikuwepo mahakamani wakati hukumu ikitolewa.
Wanasema kuwa watakata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama.
Mahakama nchini Misri pia iliamuru kufungwa kwa mashirika kadhaa yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi nchini humo likiwemo shirika la Marekani la IRI
Mwaka jana wakati Misri ilipokuwa chini ya utawala wa kijeshi,kufuatia kuondolewa mamlakani kwa aliyekuwa rais Hosni Mubarak, polisi walivamia ofisi za mashirika kadhaa ya kigeni na mengine ya Misri.
Mashirika hayo yanatuhumiwa kwa kufanya kazi bila leseni na kupokea msaada kutoka kwa mashirika yasiyojulikana.
0 Comments