Mtoto ambaye alijeruhiwa kwenye mlipuko wa bomu Arusha |
Arusha:
Mashuhuda wa tukio la mlipuko wa bomu uliotokea mwishoni mwa wiki iliyopita Jijini Arusha, wamedai kumwona na kumtambua mtu aliyehusika na tukio hilo lakini wanasema walishidwa kumkamata kutokana na “kushambuliwa kwa risasi na polisi”.
Mlipuko huo ulitokea katika Viwanja vya Soweto kwenye mkutano wa kuhitimisha kampeni za udiwani jijini humo na kusababisha vifo vya watu wanne na majeruhi zaidi ya 100.
Mashuhuda hao ambao wote walijeruhiwa kwa risasi wanasema mlipuaji wa bomu alikuwa amevalia shati la kijivu lenye mistari myeusi na suruali ya jeans yenye rangi ya blue na kwamba wajihi wake ni mtu wa kimo cha kati.
Mmoja wa mashuhuda hao ni mlinzi katika Kikosi cha Ulinzi cha Chadema (Red Brigade) ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alidai kwamba alimwona mtu aliyerusha bomu mara tu baada ya tukio hilo.
Mlinzi huyo ambaye alipigwa risasi za mguuni na kifuani wakati akimkimbiza mtu huyo, alisema bomu hilo lililipuka mara tu baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kumaliza kuhutubia na kushuka jukwaani.
“Baada ya Mwenyekiti Freeman Mbowe kushuka jukwaani, nikawapanga walinzi kwa ajili ya kuwalinda viongozi waliokuwa wakichangisha fedha. Ghafla nikasikia mlipuko, sikujua ni nini, lakini kuna mama mmoja alikuwa karibu yangu akanionyesha mtu aliyelipua, akisema yuleee…” alisema na kuongeza:
“Alikuwa amevaa shati la kijivu lenye mistari myeusi na suruali ya jeans ya blue. Ni mtu wa kimo cha kati. Watu walianza kumkimbiza kuelekea upande wa Magharibi wa Uwanja kwenye nyumba za NHC. Tuliruka uzio alipopita yule mtu, mara nikasikia risasi imenipata mguuni.”
“Tulikuwa na uwezo wa kumkakata yule mtu, lakini nikaona risasi zimezidi upande wetu nikaona nigeuze na hapo hapo nikapigwa risasi ya kifuani, nikaishiwa nguvu, sikuweza kufahamu mtu huyo alikoishia. Nilijikongoja na kurudi uwanjani.”
Mlinzi huyo ambaye amelazwa katika moja ya hospitali za jijini Arusha anasema alilazimika kuhama hospitali ya Seliani alikokuwa amelazwa awali baada ya kuandamwa na polisi. “Nilikaa siku tatu hospitalini bila kupata huduma yoyote, lakini kila siku madaktari walikuwa wakinihoji maswali,”alisema na kuongeza:
“Mwisho nikaambiwa kwamba nitahamishiwa ghorofa ya chini, nilipouliza sababu wakasema eti Waziri Mkuu atakuja kuniona… Niligoma mwisho daktari akaniambia kuwa kuna polisi waliovaa majoho ya udaktari ndiyo waliotaka nihamishwe”.
Maelezo yake yanafanana na yaliyotolewa na majeruhi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Abdallah Alila ambaye alisema kuwa alimwona mtu aliyelipua bomu “akiingia kwenye gari la polisi”.
“Baada ya mlipuko, sikujua kama nimeshapigwa risasi, lakini niliona watu wakimkimbiza mtu baada ya mama mmoja kusema kuwa ndiye aliyerusha bomu.
Watu waliokuwa wakimkimbiza walikuwa wakirushiwa risasi na polisi. Baadaye nilimwona mtu huyo akipanda gari la polisi. Nashangaa tena kusikia polisi wakimtafuta huyo mtu,” alisema Alila.
Polisi wodini
Mbali na taarifa kwamba polisi walikuwa wakizunguka katika wodi za wagonjwa wakiwa wamevalia majoho ya madaktari, pia mgonjwa mwingine amedai kwamba askari wamekuwa wakimfuatilia kila kukicha.
Peter Mshanga ambaye amelazwa katika Hospitali ya Selian hivi sasa kutokana na kujeruhiwa kwa risasi katika mguu wake wa kushoto alisema awali alipelekwa katika hospitali ya St. Elizabeth lakini alihama baada ya kuandamwa na askari kanzu.
“Mara baada ya bomu nilipelekwa Hospitali ya St. Elizabeth na huko nilishangaa kuwaona askari ninaowafahamu wakizingira kitanda changu. Hata nilipokwenda chooni askari mmoja alinifuata, nikamuuliza anataka nini, yeye akanijibu eti anataka kunisaidia, nikamkatalia akatoka nje,” alisema Mshanga na kuongeza:
“Waliendelea kuzingira kitanda changu kwa siku kadhaa, siku ya tatu daktari akasema nitakiwa nihamishiwa hospitali ya Mount Meru, nikapinga”.
Wakati huo walikuwa tayari wameandaa ambulance (gari la wagonjwa) na gari la polisi ili wanihamishe. Ndugu zangu walipinga ndipo nikahamishiwa hapa Seliani,”anasema.
Kuhusu kujeruhiwa kwake, Mshanga alisema baada ya mlipuko alishtukia ameshajeruhiwa mguuni na akaanguka chini.
“Nilikuwa nimeshika Sh500 mkononi nikisubiri kutoa sadaka yangu. Mara nikaona watoto wanaanguka mbele yangu, nikasikia kishindo kikubwa, kisha nikakimbia kubeba mmoja wa watoto, na mimi nikaanguka, kumbe nilikuwa nimejeruhiwa,” alisema.
Jana gazeti hili lilimtafuta Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas kuzungumzia suala la polisi kuwafuatilia majeruhi lakini alipopokea simu alisema hawezi kuzungumza kwa wakati huo kwa kuwa yuko kwenye kikao. “Niko kwenye kikao,” alisema Sabas na kukata simu yake.
Mkanganyiko wa taarifa
Wakati Serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu sera na Uratibu wa Bunge, William Lukuvi ikitoa kauli kuwa polisi walijihami kwa kuwapiga wananchi risasi na mabomu ya machozi, mmoja wa maofisa polisi aliyekuwa uwanjani wakati wa mlipuko ambaye pia hakutaka jina lake litajwe gazetini amekanusha kupiga watu risasi. “Mimi ndiyo nilikuwa pale uwanjani, baada ya bomu kulipuka wafuasi wa Chadema walianza kutushambulia tulipojitokeza kubeba majeruhi hadi wakavunja kioo cha gari yetu. Niliwaamuru askari warushe risasi hewani, hakuna hata mtu mmoja aliyepigwa risasi,” alisema na kuongeza.
“Unajua wafuasi wa Chadema wamelishwa chuki na viongozi wao, kama Mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema ambaye alisema akivamiwa na majambazi heri afe kuliko kumpigia simu RPC. Ndiyo maana watu walijawa chuki wakaja kutushambulia.”
Aliendelea: “Baada ya kuona mashambulizi yamezidi tukaondoka, lakini baadaye tukarudi na kukuta majeruhi wote wameshaondolewa na wafuasi wa Chadema. Baadhi ya askari kanzu waliwafuatilia majeruhi ili kujua majina na idadi yao ili tutoe taarifa”.
Kama ni risasi basi wamepigwa na viongozi wa Chadema kwani maganda mengi ya risasi yameonekana kuwa ya bastola na viongozi wao wengi wanazo,”alisema.
0 Comments