Na Waandishi Wetu SHOO mbili zilizofanyika Ijumaa iliyopita (Juni 14, mwaka huu) kwa nyakati tofauti, zimemaliza vita ya matusi iliyokuwa ikitokota kati ya wanamuziki, Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ na Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’.Lady Jaydee ambaye sasa anajiita Anaconda, alikuwa katika Ukumbi wa Nyumbani Lounge akitumbuiza mashabiki wake huku Mwana FA akiwaburudisha mashabiki wake waliofurika katika Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa, Posta, jijini Dar.SHOO YA LADY JAYDEEE Kabla ya Anaconda kupanda jukwaani, wanamuziki; Grace Matata, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, Mkoloni, Juma Kasim ‘Sir Nature’ na Wanaume Halisi pamoja na Bendi ya Bantu Group chini ya Hamza Kalala walifanya shoo nzuri ya utangulizi. Aidha wakati shoo hiyo ikiendelea, jukwaani alipandishwa swahiba wake marehemu, Albert Mangweha ‘Ngwea’, Mgaza Pembe ‘M2 The P’ akawasalimia mashabiki ndipo Anaconda alipovamia jukwaa na kufanya shoo bab’kubwa.LANGA AMTOKEA SHABIKI Wakati Lady Jaydee alipokuwa anapanda jukwaani, ghafla alisikika shabiki mmoja akipiga mayowe akisema amemuona marehemu Langa Kileo nyuma ya steji na hivyo kuzua taharuki kwa mashabiki. Jamaa huyo aliyeonekana kuchanganyikiwa alitulizwa na mabaunsa huku akiwaonesha mahali alipomuona, alipotulia Jaydee alipanda na kufanya shoo kali. Mwishoni, Jide alilifunga pazia la burudani akiwa na Legendary, Joseph Haule ‘Prof Jay’ na wimbo wa Joto Hasira.SHOO YA MWANA FA Shoo hiyo iliyokuwa na idadi maalum ya watu 400, ilikwenda kama ilivyopangwa ambapo mashabiki waliingia na kukamata siti zao kisha Mwana FA kufungua burudani kali kwa kupiga nyimbo zake ‘live’ kupitia bendi ya Njenje. Mwana FA alipiga nyimbo zake kali ikiwemo Alikufa kwa Ngoma, Unanijua Unanisikia, Mabinti na nyingine kali zilizoteka hisia za wengi.MANDOJO NA DOMOKAYA NDANI Wasanii wa kitambo, Mandojo na Domokaya walikuwa kivutio kikubwa baada ya kukaribishwa jukwaani na Mwana FA na kuimba naye wimbo wake wa Kama Zamani kisha nao wakaimba nyimbo zao kama Nikupe na Dingi zilizowakonga nyoyo mashabiki waliowatuza.WEMA KAMA KAWA Wema Sepetu naye alikuwepo ndani ya nyumba ambapo alimwagia minoti Dully Sykes kwa kuwatumia wapambe wake. Mwishoni Mwana FA alihitimisha shoo kwa kuwashukuru mashabiki wake wote akiwemo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.Shoo hizo mbili awali zilikuwa zifanyike Mei 31, mwaka huu, zikaahirishwa kutokana na msiba wa Albert Mangweha ‘Ngwea’, ulipokwisha kukawa na kurushiana matusi na mwisho ubishi ukamalizwa siku hiyo kwa kila mmoja kupiga shoo yake. Aliyefunika watu wanamjua, hakuna kumulika na tochi. Imeandikwa na: Richard Bukos, Musa Mateja, Chande Abdallah na Erick Evarist |
0 Comments