Ulinzi mkali ambao tayari upo na utazidi kuonekana wakati wa Ujio wa Rais wa Marekani umewafanya baadhi ya Watanzania kujihisi wanadunishwa au kuabishwa. Wapo wengine ambao wanaona kuwa hatua mbalimbali za kiusalama zinazochukuliwa kumlinda Obama, Familia yake na ujumbe wake zinaonesha dharau na kutoaminiwa kwa vyombo vyetu vya ulinzi. Wengine wanafika mahali pa kuhisi kuwa Wamarekani wanatudharau sana kiasi kwamba wanatuchagulia nani aonene na Obama (rejea taarifa kwenye gazeti la Mwananchi la leo). Watanzania hawapaswi kujisikia hivyo hata kidogo.
Ulinzi wa Obama ni Mkali iwe ndani ya Marekani au Nje

Wakati wowote Rais wa Marekani anaposafiri iwe ndani ya Marekani au nje ya Marekani ulinzi wake ni mkali na karibu kamili (almost absolute). Kuanzia angalia ambalo anakuwepo (linakuwa no fly zone) na kuwa anaenda na kila kitu kinachoweza kutumika wakati wowote wa dharura yoyote inayoweza kufikirika kutokea. Kuanzia majanga ya moto, maji, maandamano ya kisiasa au hata mapinduzi ya kijeshi ulinzi wa Rais wa Marekani umejiandaa.

Mfano mzuri ni kuwa ikulu ya Rais pale DC – Jumba Jeupe – juu kabisa kuna mzinga wa kutungua ndege – surface to air battery. Lakini kubwa zaidi ni kuwa anga lote linalozunguka Ikulu hiyo ni eneo ambalo ndege haziruhusiwi kuruka (prohibited airspace). Na wakati wowote Rais anaposafiri mahali popote ndege haziruhusiwi kuruka juu yake. Anapotua kwenye uwanja kwa mfano hapa Detroit, hakuna ndege nyingine itakuwa inatua wakati huo huo! Sasa kama hili linatokea Marekani kwa kiasi gani linaweza kutokea Tanzania?


Ripoti hii maalum basi ina lengo la kuwasaidia Watanzania kutokwazika na kiasi cha ulinzi ambao Obama anakuja nao pamoja na usumbufu unaotokana na hilo. Kama msafara wa Rais Kikwete huwa unazusha usumbufu kwa watu basi wa Obama utasababisha kadhia – chukua msafara wa Kikwete zidisha mara 1000!


TEMBELEA LIBENEKE LA MWANAKIJIJI KWA KUSOMA ZAIDI