NAIBU wa Rais William Ruto ameamriwa alipe faini ya Sh5 milioni kwa kuingia kinyume cha sheria katika shamba la ekari 100 la mkulima katika eneo la Uasin Gishu.
Jaji Rose Ougo pia alimwamuru Bw Ruto arudishe shamba hilo kwa mwenye Bw Adrian Muteshi.
Jaji Ougo alisema shamba hilo linamilikiwa na Bw Muteshi na kwamba “liliporwa na walaghai.” Kuamuliwa kwa mzozo huo wa shamba hilo ulitamatisha kesi ambayo iliwasilishwa kortini 2008 na wakili Antony Lubullelah.
Bw Muteshi, aliyesema kwamba alihepa kutoka shambani mwake wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi mnamo 2008  alidai Bw Ruto alifanya njama za kumnyang’anya shamba lake.
Jaji  Ougo alisema kwamba Bw  Ruto hakufika kortini kuhojiwa wakati wa kesi  hiyo  na kwamba mashahidi watatu waliofika kortini kumtetea hawakuwa wa msaada  mkubwa kisheria. Alisema kwamba Bw Ruto angelifika angelisaidia mahakama na ushahidi muhimu.
Lakini Bw Ruto kupitia kwa taarifa iliyowasilishwa na wakili wake alijitetea kwamba hakuwa na hatia na kukana kwamba alihusika katika ulaghai wa shamba hilo lilokuwa limeandikishwa kwa jina la mnunuzi Bi Dorothy Yator.
Kununua
Shahidi mkuu katika kesi hiyo, Bw Hosea Ruto alisema kwamba alifanya mkutano uliohudhuriwa na Bw Ruto na wanaume  wawili Mabw Peter Kosgei na Bethwell Kipsang.

Makubaliano yalifikiwa kwamba Bw Ruto atanunua shamba hilo. Wakati huo Bw Ruto alikuwa Waziri wa Kilimo.

Akimtetea Bw Ruto wakili Katwa Kigen alisema kwamba naibu huyu wa rais hakununua shamba hilo akitaka kumtendea hila mlalamishi.

Alisema Bw Ruto alinunua shamba kwa kuelewa kwamba alikuwa anafuata sheria.