Mwanamama akipita katika ukuta wenye picha ya Nelson Mandela mjini Soweto. Mandela anapatiwa matibabu huko Pretoria na hali yake inaelezwa kuwa ni mahututi na wananchi wamekuwa wakimwombea nafuu ya haraka. Picha ya AFP 

Habari zilizotapakaa katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Johannesburg ni kwamba hakuna matumaini ya Mandela kupona na sasa familia yake inajadiliana kuhusu taratibu za mazishi yake huku mwenyewe akiendelea kupumua kwa msaada mashine hospitalini alikolazwa.

Mandela (94) amelazwa katika Hospitali ya Magonjwa ya Moyo, Med – Clinic, Pretoria kwa siku ya 19 sasa na taarifa ambazo zimekuwa zikitolewa na Ikulu ya Afrika Kusini tangu Jumapili, usiku zinathibitisha kwamba hali yake ni mahututi.

“Tunasubiri habari mbaya za kifo cha Mandela maana taarifa zinazotolewa na Serikali kuhusu hali ya afya yake ni dalili kwamba hawezi kuishi tena,” alisema mkazi wa Johannesburg, Doroth Nyathi alipozungumza na mwandishi wetu na kuongeza:
“Watu wanaamini kwamba Mandela ameshafariki dunia, lakini Serikali na familia yake wanatuficha tu, labda wanasubiri maadhimisho ya siku yake ya kuzaliwa mwezi ujao.”

Mandela anafikisha umri wa miaka 95 Julai 18 mwaka huu, lakini kuna wasiwasi kwamba huenda asiifikie siku hiyo ambayo ni maarufu kama “Mandela Day” kutokana na kuzorota kwa afya yake.

“Kama mtu hajafa mnawezaje kukaa kujadili mahali pa kumzika, ndiyo maana nimekwambia ni dhahiri kwamba Mzee Madiba (Mandela) tayari amefariki, ila wanatuficha tu,” alisema Nyathi.
Nyathi alikuwa akirejea taarifa za vyombo vya habari kwamba familia ya Mzee Mandela ilikutana katika kikao cha siri juzi kati ya saa 5:00 asubuhi na saa 08:00 mchana kujadili “mahali pa maziko” ya shujaa huyo aliyeongoza mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi, kufungwa jela miaka 27 na baadaye kuwa Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini.

Habari kutoka katika kikao hicho kilichohudhuriwa na waziri katika Serikali ya Afrika Kusini ambaye pia ni mwanafamilia wa Mandela na mmoja wa viongozi wa vyama vya siasa, zinasema baadhi walikuwa wakitaka azikwe alikozaliwa huko Mvezo, wakati wengine wakitaka azikwe Qunu.

Baadhi ya vyombo vya habari vya Afrika Kusini vimesema Mandela atazikwa Qunu, taarifa ambazo hata hivyo, hazijathibitishwa na Serikali ya Afrika Kusini ambayo imekuwa ikisisitiza kwamba “Familia ya Mandela isaidiwe katika kipindi hiki kigumu.”

Kwa upande wake, mkazi wa Pretoria, Lisa Wright alisema wasingependa kumpoteza Mandela lakini kwa jinsi hali inavyoendelea ni dhahiri kwamba maradhi yanamzidi nguvu hasa kutokana na umri mkubwa.

“Tutamkumbuka sana Mzee Mandela, amechangia kufuta uhasama baina ya watu weupe na weusi hasa kutokana na moyo wake wa kusamehe baada ya kutoka gerezani, hivi leo suala siasa za ubaguzi litageuka historia hasa baada ya kizazi hiki kupita,” alisema Lisa.

Hali ilivyo nyumbani
Nyumbani kwa Mandela, eneo la Houghton, Mtaa wa Laan 12 jijini Johannesburg, watu kwa makundi wamekuwa wakifika na kuweka maua kwenye vitalu vinavyozunguka makazi yake na wengine wakiandakia ujumbe wa kumtakia heri ya kupona haraka kwenye mawe madogomadogo yaliyoko kwenye vitalu hivyo.

Makazi hayo pia yamezungukwa na magari yanayotumiwa na waandishi wa habari kutoka nchi mbalimbali, ambao kwa zaidi ya wiki tatu wameweka kambi katika eneo hilo tangu kuripotiwa kuzorota kwa afya ya kiongozi huyo.