Alisema, “Inasikitisha sana ila imeshatokea yaani marehemu amefariki saa moja kabla ya ndoa yake na baada ya kifo hicho, mtoto wake naye alifariki muda mfupi baada ya mama yake kufariki dunia,” alisema Mrimasha.
Akizungumzia mkasa huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Harusi hiyo iliyogharimu Sh7.7 milioni, Abdi Kipacha alisema kuwa kwake ni tukio la kwanza kutokea tangu kuzaliwa kwake na kamwe hawezi kulisahau.
“Nilishazipangia kazi kamati za maandalizi, lakini ghafla tukapewa taarifa kuwa bibi harusi amefariki...Hatukuamini, ikabidi niwatangazie wanakamati wenzangu kuwa hakuna tena shughuli, bibi harusi amefariki,” alisema mwenyekiti huyo wa kamati na kuongeza:
“Kitu tulichokuwa tukisubiri ni kuambiwa bibi harusi angefika saa ngapi, lakini ghafla tukapewa taarifa za kifo, ilikuwa ni vigumu kuamini lakini ni kweli imetokea na inasikitisha kwani si jambo la kawaida,” alisema Kipacha.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na wanandugu ni kuwa marehemu alikuwa Mwalimu wa Shule ya Msingi Nndawa mkoani Lindi na kwamba alikuwa katika kundi la walimu wa ajira mpya ambayo hadi mauti yanamkuta alikuwa hajapokea hata mshahara wake wa awali.
Akizungumzia hali hiyo, Padri aliyekuwa afungishe ndoa hiyo, Max Sabuni wa kanisa hilo Katoliki Handeni alisema: “Nimesikitishwa na tukio hili kwa kuwa halikuwahi kunitokea...Kilichobaki ni wanandugu kuwa watulivu kwa kuwa Mungu amechukua kiumbe wake kwa muda alioupanga.”
Aliwataka ndugu, jamaa na marafiki kuwa na subira katika kipindi hiki cha majonzi.Naye mume wa marehemu, Kasisi Masawe alisema: “Nimechanganyikiwa sana na hili...Ni jambo ambalo sikulitarajia. Ninamshukuru Mungu kwa yote japokuwa kifo hiki kimeniharibia mipango yangu mingi ya maisha na Levina.
“Nilipanga mengi na yeye, lakini Mungu hakupenda...Nilimpenda sana Levina,leo ameniacha. Amekwenda na mwanangu...Ni pigo kubwa kwa kweli, mke na mtoto kwa wakati mmoja, inauma sana.”
Mwili wa bibi harusi huyo ulisafirishwa jana kupelekwa Machame mkoani Kilimanjaro kwa maziko ambayo yanafanyika leo Jumatano pamoja na mtoto wake ambaye naye alifariki saa chache baada ya mama yake.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Costantine Massawe alithibitisha kutokea tukio hilo lakini akasema hawezi kuzungumzia kwa undani kwa kuwa ni tukio la kifamilia zaidi.
---------------------------------
Na Rajabu Athumani. Mwananchi
0 Comments