Wananchi wakifuatilia mkutano wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana.
-POLISI WATHIBITISHA KULILIPUKA
-LAKINI WADAI NI BAHATI MBAYA
Ikiwa ni takribani mwezi mmoja tu tangu bomu lilipolipuka kwenye mkutano wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mkoani Arusha, jana tukio kama hilo lilitokea jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, ambao aliutishia kwa lengo la kuwaelezea wananchi mrejesho wa yaliyojiri bungeni hivi karibuni na kuhamasisha wananchi kushiriki kutoa maoni kwenye rasimu ya Katiba mpya.
Tofauti na Arusha, jana bomu hilo lililipuka likiwa kwenye gari la Polisi waliokuwa kwenye mkutano huo katika viwanja vya Sahara, katika Kata ya Mabibo jijini Dar es Salaam na kuibua taharuki kubwa kwa wananchi na wafuasi wa Chadema waliokuwa wamehudhuria mkutano huo.
Polisi wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kwamba bomu hilo lililipuka kwa bahati mbaya na kwamba ni la jeshi hilo.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Kinondoni, Yusuf Mrefu, alisema mlipuko huo ulitokea kwa bahati mbaya na kwamba haikuwa nia ya polisi kutumia nguvu au kuzuia mkutano wa Chadema.
"Ni bomu la mkononi. Polisi walikuwa na mazungumzo na viongozi wa Chadema na siyo kwamba kulikuwa na vurugu au matumizi ya nguvu, ni tukio la bahati mbaya," alisema.
Mrefu alisema pia kwamba Polisi haikuwa imepanga kupiga mabomu kwenye mkutano huo wala kuuzuia.

"Siwezi kueleza limetengenezwa wapi, ni aina gani au kazi yake; kwa sababu mimi mwenyewe nimepewa taarifa kwa simu, sikuwa eneo la tukio, nilikuwa kwenye msafara wa Makamu wa Rais," alisema.

Aidha, Kaimu Kamanda huyo bila kufafanua alisema: "Halina madhara." Hata hivyo, alipoulizwa kazi ya bomu hilo ikiwa halina madhara, alijibu kwamba asingeweza kueleza zaidi kwa kuwa hakuwa na taarifa za kina kwa kuwa hakuwa eneo la tukio.

Hata alipoulizwa jina la kitaalamu la bomu hilo alisema hana taarifa za kina.

Wakati Polisi wakieleza hayo, mashuhuda pamoja na taarifa zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilidai kwamba mtu mmoja alijeruhiwa kwenye tukio hilo.

Taarifa zinaeleza kwamba mlipuko huo ulitokea baada ya Mnyika kwenda kwenye gari ya Polisi kwa nia ya kuwasalimia na ndipo kishindo kilichoashiria mlipuko wa bomu kilisikika.

Kufuatia tukio hilo, mkutano huo ulipigwa marufuku na kuhamishiwa eneo la Ubungo Mataa ambako ulifanyika.

 Diwani wa Ubungo (Chadema), Boniface Jacob, akifungua mkutano huo alisema waliamua kuchukua vibali viwili vya mkutano huo kwa tahadhari cha Mabibo na cha Ubungo.

Akizungumzia kuhusu tukio hilo wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Ubungo jana, Mnyika alidai kuwa waliomba kibali cha kufanya mkutano huo siku tano kabla kwa kuwaandikia polisi barua, lakini hawakuwajibu hadi jana asubuhi wakiwataka kusitisha kwa sababu kulikuwa na ziara ya Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, kukagua shughuli za usafi jijini Dar es Salaam.

Mnyika alisema aliwajibu polisi kuwa hawezi kupokea taarifa za kusitisha mkutano wake huyo kwa simu bali aliwataka wampe kwa maandishi.

Alisema baadaye polisi waliandika barua ya kumuagiza asitishe mkutano wake huo kupisha ziara ya Makamu wa Rais.

Alisema hata hivyo, alipoangalia ratiba ya ziara ya Makamu wa Rais, aligundua kuwa haikugusa jimboni mwake na kuwaomba tena polisi wamruhusu kufanya mkutano huo.

Alisema alimtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Suleiman Kova na kujibiwa yuko nje ya nchi, hivyo aliwaomba wasaidizi wake wampe kibali lakini hawamkujibu na kumuomba asubiri wajadiliane kwanza.

Mnyika alisema kutokana na muda kuyoyoma, alimtafuta Mkuu wa Jesh la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Said Mwema, kumuomba amsaidie, lakini aligonga mwamba baada ya kumjibu kuwa hawezi kutengua maamuzi yaliyotolewa na kiongozi wake wa chini na kumtaka aandike barua nyingine ya kuomba kibali cha kufanya mkutano.

"Wakati naendelea kuwasiliana na viongozi wa polisi kuomba wanipe kibali, nilikuwa tayari kwenye viwanja vya Sahara na ndipo zikaja defender (magari ya polisi) tatu za polisi," alisema na kuongeza kuwa:

"Ziliposimama niliwafuata na kwenda kuwaambia kuwa vipi tena mbona mmekuja wakati nimeomba kibali cha kufanya mkutano, ndipo lilipolipuka bomu hilo ndani ya gari ambalo nami nilikuwa nimesimama karibu nalo."

Alisema baada ya kulipuka bomu hilo, watu walikuwa wamekusanyika katika viwanja hivyo walikumbwa na taharuki na kukimbia ovyo kunusuru ya maisha yao. Kwa mujibu wa Mnyika, wakati watu hao wakikimbia ovyo, alikwenda lilikoangukia bomu hilo kumuwahi majeruhi, Thomas Jarome.

Alisema polisi nao walikwenda kumuwahi majeruhi huyo na kumbeba 'mzobemzobe' wakati wakitaka kumuingiza kwenda gari lao, Mnyika na viongozi wengine wa Chadema waliwazuia na kumpeleka hospitalini ambako alipatiwa matibabu na kuruhusiwa kuondoka.

Alisema wakati majeruhi huyo akiendelea kupatiwa matibabu, viongozi wa chama hicho walikusanyika na kujadili sehemu nyingine ya kwenda kufanyia mkutano wao na kubaini kuwa Diwani wao wa Ubungo alikuwa na kibali cha kufanya mkutano eneo la Abiani Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Aliwatangazia wananchi wafuasi na wapenzi wa Chadema wakiwaomba wahamie Abiani.

Katibu wa Mbunge wa Ubungo, Gastone Garubindi, alidai bomu hilo lilipigwa na polisi kwa lengo la kuwatisha wananchi wasihudhurie mkutano huo.

Akizungumza na NIPASHE majeruhi Jerome, alidai kuwa polisi walikusudia kulipua bomu hilo kwani lilikuwa mikononi mwao na askari waliopata mafunzo ya kutosha kuhusu milipuko.

Alisema baada ya kujeruhiwa, viongozi wa Chadema walimpeleka katika kituo Mabibo ambako alipewa PF3 na kwenda zahanati Tandale na kutibiwa.

Jerome alisema baada ya kutibiwa aliruhusiwa kurejea nyumbani na kutakiwa kurudi leo kwa uchunguzi zaidi na kuchomwa sindano ya pepopunda (tetanus).

Tukio la jana limekuja huku uchunguzi wa mlipuko wa bomu uliotokea Juni 15, mwaka huu katika viwanja vya Soweto, Kata ya Kaloleni mkoani Arusha kwenye mkutano wa kufunga kampeni za udiwani wa Chadema, ukiwa bado unaendelea. Katika tukio hilo, watu watatu walipoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa vibaya. Bomu hilo linaelezwa kuwa lilipuka kwenye mkusanyiko wa watu mita chache kutoka jukwa kuu, wakati mkutano huo ulipokuwa umekwisha na shughuli ya kukusanya michango ikiendelea.

Viongozi wa juu wa Chadema, Freeman Mbowe na Godbless Lema walikuwapo kwenye eneo hilo.

Hadi sasa hakuna mtu ambaye amekamatwa kuhusiana na mlipuko huo pamoja na kwamba Serikali imetangaza donge nono la Sh. milioni 100 kwa mtu atakayefanikisha kukamatwa kwa mhusika au wahusika wa tukio hilo.

Zaidi ya watu 70 walijeruhiwa baada ya tukio hilo kufuatia polisi kufyatua risasi za moto kwa nia ya kukabiliana na wananchi waliokuwa wanawashambulia.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alikaririwa akieleza kwamba bomu lililolipuka Arusha lilitengenezwa China.

Aidha, Septemba, 2012 aliyekuwa Mwakilishi wa Kituo cha Chanel Ten mkoani Iringa, Daudi Mwangosi, aliuawa kwa kupigwa bomu la machozi na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) eneo la Nyololo Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.

Alipigwa bomu hilo baada ya kupokea kipigo kutoka kwa baadhi ya askari wa FFU waliokuwa wakiizuia Chadema kuendesha harakati zake za kufungua tawi la chama hicho katika eneo hilo.

Mwangosi ambaye pia alikuwa  Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC), aliuawa mbele ya wananchi, askari wa FFU na aliyekuwa  Kamanda wa jeshi hilo mkoani humo, Michael Kamuhanda.

Askari huyo anayedaiwa kumuua Mwangosi, Pacificus Cleophase Simon (23), alikamatwa na kufikishwa mahakamani akikabiliwa na tuhuma za mauaji hayo na kesi hiyo bado inaendelea kutajwa.

CHANZO: NIPASHE