Mchuuzi wa maboga sokoni akiyaweka tayari kwa kuyauza jijini Dar es Salaam. Picha na Maktaba.

Dar es salaam. Bei za vyakula katika baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam zinazidi kupaa kipindi hiki cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani .

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili maeneo ya Tabata Kimanga, Bima na hata Segerea umeshuhudia bidhaa za vyakula zikiwa juu ukilinganisha na maeneo ya Kariakoo, Vingunguti na hata Magomeni.

Bei ya kilo moja ya nyama maeneo ya Tabata ni Sh6,500 wakati maeneo ya Vingunguti ni Sh5,000 huku Kariakoo ikiwa ni Sh5,500.

Bidhaa kama magimbi,viazi zinadaiwa kupanda kutokana na ugumu wa upatikanaje wake katika masoko kwa mujibu wa mfanyabiashara wa soko la Buguruni, Omari othumani.

“Kwa kipindi hiki mahitaji ni makubwa kuliko upatikanaji wa bidhaa,hali hii imesababishwa na mvua kutokunyesha kwa wakati na kusababisha uhaba wa mavuno,”alisema Othumani.Alisema wakulima ndiyo chanzo kikuu cha bei kupanda kwani wanauza kiroba kimoja cha magimbi na viazi shambani kwa Sh50,000 lakini wafanyabiashara wa jumla hulazimika kuuza kwa Sh90,000 ili kufidia ushuru na gharama za usafilishaji.