Picha ya Nelson Mandela na maua iliyoachwa nje ya hospitali na
watu waliofika kumfariji.
Mke wa Nelson Mandela, Graca Machel amesema kwa sasa hana wasi
wasi sana kuhusu afya ya rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini kama ilivyokuwa
wiki chache zilizopita.
Bi Machel amesema hali ya Mandela inaendelea kuimarika kila uchao.
Mandela ambaye ni rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, mwenye umri wa
miaka tisini na nne, anasemekana kuwa katika hali mahututi.
Mandela alilazwa hospitalini wiki tano zilizopita na hapo jana rais wa Afrika
Kusini, Jacob Zuma, alisema kuwa mwanaharakati huyo wa uhuru amesalia kuwa
mpiganiaji mkubwa kama alivyokuwa miaka hasmini iliyopita.
Mandela alilazwa hospitalini tarehe nane mwezi Juni, kutokana na maambukizi
ya mapafu.
Wiki iliyopita, rais Zuma alipuuzilia mbali madai kuwa afya ya Bwana Mandela
imezorota kiasi kwamba hawezi kupona tena.
Watu kadhaa ambao wamemtembela hospitalini wamesema kuwa Bwana Mandela angali
ana ufahamu na anaweza kujibu na kuitikia salamu.
Mwandishi wa BBC Mjini Johannesburg, amesema kuwa Bi. Machel amekuwa kando ya
mumewe tangu alipolazwa hospitalini na amejiepusha na mzozo unaokumba familia ya
Bwana Mandela kwa wiki kadhaa zilizopita.
Maafisa wa serikali ya Afrika Kusini wametoa wito kwa raia wa nchi hiyo
kujiandaa kwa sherehe za kuadhimisha miaka tisini na tano ya kuzaliwa kwa Bwana
Mandela wiki ijayo.
Mandela anaenziwa kote duniani kutokana na juhudi zake za kumaliza utawala wa
ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.
Alifungwa miaka 27 gerezani kabla ya kuachiliwa huru mwaka wa 1990 na
kuchaguliwa kuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini mwaka wa 1994. |
0 Comments