Dar/Geneva.
 Wakati miili ya wanajeshi saba wa Tanzania waliouawa nchini Sudan ikiwasili leo, taarifa zinadai kundi la Janjaweed ambalo linaungwa mkono na Serikali, linahusika katika mauaji hayo.

Wanajeshi hao wa Tanzania ambao ni sehemu ya Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa (Unamid), waliuawa Julai 13 eneo la Kusini mwa Darfur.

Askari wengine 17 walijeruhiwa katika shambulio hilo na wanaendelea kupatiwa matibabu kwenye hospitali maalumu.

Taarifa za UN, zilieleza juzi kwamba ingawa kundi hilo halijatambuliwa rasmi, mashuhuda wamekuwa wakieleza mauaji hayo yamefanywa na kundi linaloungwa mkono na Serikali ya Sudan.
Kiongozi wa moja ya makundi ya wapiganaji la Sudan Liberation Movement (SLM), Minni Minnawi, ndiye aliyeibuka awali na kuwatuhumu mgambo wanaoungwa mkono na Serikali na kutaka ufanyike uchunguzi wa kimataifa.

Katika mahojiano yake na gazeti la Sudan Tribune alipokuwa akihudhuria mkutano wa majadiliano kuhusu namna ya kupata amani ya kudumu nchini Sudan uliofanyika mjini Geneva, Uswisi, Minnawi alikanusha tuhuma kwamba kundi lake linahusika na shambulio hilo.

Kiongozi huyo alikuwa akijibu tuhuma za Serikali ya Sudan kwamba, kundi lake ndilo lililohusika na shambulio hilo.
“Tuna uhakika shambulio lililofanywa dhidi ya walinzi wa amani wa Unamid liliandaliwa na kutekelezwa na Janjaweed, tuko tayari kutoa ushirikiano kwa chombo maalumu cha kimataifa kitakachoundwa kufanya uchunguzi kuhusu tukio hili,” alisema.

Alisema wanamgambo wa Janjaweed hivi sasa wanakabiliwa na ukata wa hali ya juu na ukosefu wa vifaa, kwa sababu Serikali haina tena uwezo wa kuwafadhili hivyo wameamua kufanya matukio ya uporaji kukidhi mahitaji yao.

Wanajeshi saba waliuawa kwenye shambulio lililotokea Julai 13 huko Khor Abeche, Nyala nchini Sudan wakati walinda amani.

Wakati huohuo, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limesema miili ya wanajeshi hao itawasili leo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, (Terminal one) saa 9:00 alasiri.

“Baada ya kuwasili miili hiyo itapelekwa Hospitali ya Kuu ya Jeshi, Lugalo. Baada ya maandalizi, miili hiyo itaagwa rasmi kwa heshima zote Jumatatu kuanzia saa 3:00 asubuhi viwanja vya Wizara ya Ulinzi, Upanga, Dar es Salaam,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.Katika hatua nyingine, Msemaji wa Katibu Mkuu wa UN, Martin Nesirky, alisema walinda amani hao waliwekewa mtego wakiwa katika majukumu yao ya msingi ya kulinda amani. Alisema UN imeanza kufanya uchunguzi wake binafsi na kuitaka Serikali ya Sudan kuwasaka wahusika ili wawajibishwe.