Shirika la kutetea haki za kibinadamu la Human Rights Watch limesema kuwa kundi
la wapiganaji la M23 Mashariki mwa Jamhuri ya Demokrsia ya Congo limewaua zaidi
ya watu arobaini na kuwabaka zaidi ya wanawake na wasichana sitini tangu Machi
mwaka huu.Baada ya kuwahoji zaidi ya watu mia moja eneo hilo, shirika hilo lilisema kuwa
waasi hao wanawasajili kwa nguvu vijana huko DRC na wengine kutoka nchi jirani
ya Rwanda.Kundi hilo limeongeza kuwa Jeshi la Rwanda bado linawasadia moja kwa moja
waasi hao licha ya serikali ya Kigali kupinga hilo mara kwa mara.
Wakati huohuo, jeshi la DRC hapo jana lilishambulia ngome za waasi hao karibu
na mji wa Goma Mashariki mwa DRC.
Haya yalikuwa mashambulizi ya kwanza tangu vita kati ya pande hizo mbili
kuanza Jumatatu asubuhi na kusitishwa siku hiyo mchana.
Kundi hilo limesema liko umbali wa kilomita nne kutoka mji wa Goma, ingawa
limesema lengo lake ni kulazimisha serikali kufanya mazungumzo nao wala sio
kuteka mji wa Goma.
M23 liliuteka mji wa Goma, kwa siku kumi mwezi Novemba kabla ya kuondoka
mjini humo kufuatia shinikizo za jamii ya kimataifa kufanya mazungumzo na
serikali ya rais Joseph Kabila.
Mazungumzo na serikali yalianza mjini Kampala mwezi Disemba ingawa baada ya
miezi miwili jeshi likaanza tena mapigano na waasi hao mwezi Julai tarehe 14.
Kulingana na Umoja wa Mataifa mapigano hayo yamesababisha takriban watu 4,200
kutoroka makwao. |
0 Comments