Dar es Salaam.
 Rais wa Marekani, Barack Obama na mwenyeji wake, Rais Jakaye Kikwete walionyesha umahiri wao wa kusakata soka lakini kwa kutumia mpira usiokuwa wa kawaida.
Viongozi hao walikuwa kivutio jana kwenye eneo la mtambo wa kufua umeme wa Kampuni ya Symbiom wa Marekani.
Rais Obama alitembelea mtambo huo ulioko eneo la Ubungo, Dar es Salaam, ambako alitangaza mpango wa kusambaza umeme kwa nchi mbalimbali za Afrika unaoitwa Power Africa.
Viongozi hao walionyeshwa mpira huo, ambao uko sawa na ile inayotumika kwenye mechi za soka lakini unatumika kama chaja ya simu au umeme.
Mpira huo unaofanya kazi vizuri zaidi baada ya kuchezewa, uligunduliwa na wanafunzi wawili wa Chuo Kikuu cha Harvard cha Marekani.
Rais Obama ndiye alikuwa wa kwanza kuchukua mpira huo na akaurusha juu na kuudaka halafu akaurusha juu na kuupiga kichwa mara kadhaa.
Baadaye alitoa pasi kwa Rais Kikwete, ambaye alitoa pasi kwa Obama na kupasiana kwa muda.

Rais Obama alihoji bei ya mpira huo na alitaka kujua nguvu ya umeme inayotolewa na mpira ule.

“Kuna chombo ndani cha kuzalisha umeme. Kadiri mpira huu unavyopigwa ndiyo unatoa nguvu sawa na betri,” alisema mmoja wa viongozi wa Symbiom wakati akitoa maelezo kwa Marais Obama na Kikwete.

Hata hivyo, mpira huo ukichezewa kwa dakika 30 basi unakuwa na nguvu ya kutosha ya kufanya kazi ya chaja.

Rais Obama alisema ugawaji wa mipira ni sehemu ya mpango wake wa kusambaza umeme barani Afrika.
------------------------------

MWANANCHI