MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amejisalimisha polisi. Mbowe alijisalimisha polisi jana saa 8.00 mchana makao makuu ya Polisi Dar es Salaam na kuhojiwa na kikosi maalumu cha makachero wa jeshi hilo.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willbrod Slaa, alithibitisha Mbowe kujisalimisha polisi akiwa amefuatana na mwanasheria, Nyaronyo Kicheere.
“Si kweli kwamba Mbowe amekamatwa, amekwenda polisi mwenyewe. Kama nilivyoeleza kwenye mkutano wetu pale Manzese juzi…Polisi walikwenda nyumbani kwake Mikocheni usiku kwa ajili ya kumkamata hawakufanikiwa.
“Siwezi kusema anahojiwa au vipi, bali ameenda huko kama tulivyokubaliana,” alisema Dk. Slaa.
Hatua ya Mbowe kujisalimisha imetokana na tarifa kuwa polisi walivamia nyumbani kwake saa 6.00 usiku Ijumaa iliyopita kwa lengo la kumkamata.
Chanzo cha kuaminika kutoka makao makuu ya polisi, kilisema Mbowe alihojiwa kwa tuhuma mbalimbali zikiwamo za uchochezi anaoufanya kwa kujenga chuki kati ya wananchi na polisi.
Chanzo hicho kilisema tuhuma nyingine ni kauli yake aliyowahi kuitoa kuwa polisi inahusika katika tukio la mlipuko wa bomu uliotokea Juni 15 mwaka huu CHADEMA walipokuwa wakihitimisha mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo kwenye viwanja vya Soweto mjini Arusha.
Katika tukio hilo,watu wanne walikufa na wengine kadhaa kujeruhiwa vibaya katika tukio hilo.
Katika tukio hilo,Mbowe alidai Chadema kina ushahidi wa kutosha kuwa polisi wanahusika na tukio hilo kutokana na kuwa na mkanda wa video unaoonyesha tukio zima.
Lengo la kufanya hivyo linadaiwa kuwa ni kukidhoofisha chama hicho na kukisaidia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi wa madiwani Arusha.
Tuhuma nyingine ambayo Mbowe alihojiwa ni kuhusiana na kauli yake kuwa kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kutohudhuria mazishi ya watu waliofariki dunia katika mlipuko huo,kilihusishwa moja kwa moja kuwa ni ishara ya jeshi hilo kuhusika katika mauaji hayo.
Habari zaidi zinasema Mbowe anatuhumiwa kulichafua Jeshi la Polisi la Tanzania kwa kile alichodai ni moja ya jeshi katili Afrika Mashariki.
Chanzo chetu kilisema tuhuma nyingine ni uchochezi anaoufanya kuhusiana na kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyoitoa bungeni hivi karibuni.
Katika kauli hiyo, Pinda alisema alilielekeza jeshi la polisi kuwashughulikia watu wasiotii sheria.
USHINDI
Katika hatua nyingine, CHADEMA kimesema kimefutwa machozi baada ya kuibuka na ushindi wa udiwani katika uchaguzi mdogo wa kata nne mkoani Arusha kutokana na matukio makubwa yaliyotokea mkoani humo.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho,John Manyika alisema ushindi huo umeonyesha wazi jinsi wananchi wa Mkoa wa Arusha, walivyo tayari kubadili hali ya siasa, licha ya kupambana na vikwazo vingi.
Alisema ushindi huo ni heshima kwa watu waliouawa wakati wakisimamia mabadiliko na haki katika taifa.
Alisema ushindi huo ni ushahidi tosha kwamba mabomu na risasi za polisi haziwezi kuzuia mabadiliko na mamlaka ya wananchi kupitia sanduku la kura.ARUSHA
Habari kutoka mkoani Arusha zinasema hali ya hewa katika Jiji hilo nusura iharibike, baada ya polisi waliokuwa na mabomu ya machozi kushindwa kuwatawanya wafuasi wa CHADEMA.
Hali hiyo ilitokea baada ya msafara wa viongozi wa chama hicho, wakiongozwa na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema walikuwa wakiwasindikiza madiwani wateule hadi ofisi za Manispaa ya Jiji la Arusha kwa ajili ya kujitambulisha.
Lema na madiwani wateule walikuwa wakitokea kwenye ofisi zao zilizopo eneo la Kilombero umati wa watu ulijitokeza kuwasindikiza.
Msafara huo ulitawaliwa na nderemo, vifijo, honi za magari, pikipiki na baiskeli.
Katika eneo hilo, polisi walilazimika kuegesha magari yao yakiwa yamejaza askari wengi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU).
Baada ya vuta nkuvute, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha (OCD), Gilles Mroto alilazimika kumfuata Lema na kumuomba awatulize wafuasi wake.
Baada ya kufanya mazungumzo hayo kwa takriban robo saa, ndipo Lema aliporejea kwa wafuasi wake na kuwataka kuwa watulivu.
“Peoples Powers… makamanda n nawaomba mtawanyike tutawatangazia siku maalumu ya kuwapa shukrani zetu kwa kazi nzuri.
Mbali ya Lema, wabunge wengine waliokuwapo ni Mbunge wa Arumeru Mashariki,Joshua Nassari, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Arusha,Joyce Munkya, Mbunge wa Karatu, Mchungaji Israel Natse.
Madiwani wateule ni Jeremiah Mpiga (Elarai),Mchungaji Rayson Ngowi (Kimandolu),Kessy Lewi (Kaloreni) na Kinabop Edmound (Themi).
0 Comments