Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete akisalimiana na Rais wa Malawi Joyce Banda 

Blantyre. Rais wa Malawi, Joyce Banda amewaambia Marais wa zamani wa Msumbiji na Afrika Kusini hakuna cha kuzungumza kuhusiana na mzozo wa Ziwa Nyasa.

Joachim Chissano na Thabo Mbeki walikwenda Lilongwe kwa ajili ya mazungumzo kuhusu mzozo wa mpaka wa Malawi na Tanzania.

Nchi hizo mbili ziliuwasilisha mzozo huo kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Uchumi Kusini mwa Afrika(Sadc), ambayo kwa sasa iko chini ya Chissano.

Akizungumza jana Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, alisema: “Wao [Chissano na Mbeki] walikwenda Malawi kwa mazungumzo hayo sasa tunasubiri watakapokuja, tutazungumza.”
Katika mkutano wa kwanza uliofanyika Tanzania, mawaziri wa mambo ya nje walifikia muafaka wa kukubaliana kutokukubaliana kuhusu suala hilo na kuliwasilisha kwa viongozi wa zamani wa Sadc kwa ajili ya maridhiano.

Rais Banda alimwambia Chissano pia kuwa katika majadiliano hayo, endapo Malawi itaona hairidhishwi na mwenendo wa majadiliano, italipeleka suala hilo mahakama za kimataifa.

source