Basi la kampuni ya Sumry limetumbukia mtoni na kusabisha watu tisa kupoteza maisha na kujeruhi abiria wapatao 53 katika mto Iku uliopo katika kijiji cha Sitalike wilaya ya Mlele mkoani Katavi
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea saa sita usiku kuamkia Julai 5, 2013 wakati basi hilo lilipokuwa likitokea mjini Sumbawanga kuelekea Mpanda mkoani Katavi likiwa na abiri waliokuwa wametoka Mbeya.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Katavi Emanuely Nnley alisema kuwa ajali hiyo ilihusisha basi aina ya Nissan Diesel lenye namba T909 AZT mali ya kampuni ya Sumry lililokuwa likiendesha na dereva aliyetajwa kwa jina na Stephano Chimane maarufu kwa jina la Ntungu.
Mganga mkuu wa wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi, Dr Emanuely Kamgobe alisema basi hilo lilipofika katika daraja hilo lenye kona kali na mteremko dereva wake alishindwa kulenga daraja hali iliyosababisha tairi za nyuma kupanda juu ya ukingo na kudumbukia mtoni ambapo dereva huyo alitoka na kukimbilia kusikojulikana.
Alifafanua kuwa juhudi za uokoaji zilianza kufanyika usiku huo huo ambapo majeruhi 53 waliokolewa na maiti tisa za wanaume watatu na wanawake watano na mtoto mmoja wa kike ziliopolewa katika maji
Alisema hali ya majeruhi inaendelea vizuri isipokuwa majeruhi watatu walikimbizwa katika hospitali ya mkoa wa Rukwa kwa matibabu zaidi na kufafanua kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva kushindwa kuliongoza gari, ubovu wa gari na wembamba wa daraja
Afisa Mwandamizi wa SUMATRA mikoa ya Rukwa na Katavi, David Chiragi alisema basi hilo lilikuwa limeiba njia kwani leseni yake inaliruhusu basi hilo kufanya safari za Sumbawanga Kirando na siyo Sumbawanga Mpanda kwa mujibu wa leseni iliyotolewa mwezi Juni mwaka huu
Alisema hata upana wa daraja ilipotkea ajali hiyo ni mdogo sana ambapo vipimo vinaonesha daraja hilo lina upana wa mita 3.5 (tatu na nusu) tu wakati basi lina upana wa mita nne na nusu hivyo kujenga mazingira ya ugumu wa dereva kulenga daraja inapotokea msukosuko wa aina yoyote hasa wakati wa usiku na hivyo kuwataka wakala wa barabara mkoani Katavi kuangalia namna ya kupanua daraja hilo na kuboresha eneo hilo
Alisema katika kipindi cha Januari hadi July 2013 zaidi ya ajali tisa zimetokea katika daraja hilo zikihusisha magari makubwa saba na madogo mawili kutokana na madereva kushindwa kumudu magari yao na kulenga daraja hilo
Alisema pia basi hilo lina makosa ya kutembea nje ya ratiba, kuiba njia na kuzidisha abiria hivyo ofisi yake imechukua hatua ya kuvunja safari za mabasi ya kampuni ya Sumry za mchana na badala yake mabasi yote yataondoka Sumbawanga na Mpanda majira ya asubuhi pekee. [picha na habari kwa ihsani ya Michuzi] |
0 Comments