Mwana Mfalme Prince William akiwa na Mkewe.
Mke wa mjukuu wa mfalme wa Uingereza, Prince William
amejifungua mtoto wa kiume katika hospitali ya St.Mary's, Paddington Mashariki
mwa mji wa London.
Katika taarifa ya Kasri la kifalme la Kensington, Duchess wa Cambridge
amepata mtoto wake wa kwanza majira ya saa kumi na dakika ishirini na nne za
jioni kwa saa Uingereza,akiwa amezaliwa na kilo 3.62874.
Kasri la Kifalme limesema, mama na mwanawe wanaendelea vyema na watasalia
hospitalini usiku huu.
Baba wa Mtoto, Prince William alishuhudia wakati mtoto akizaliwa.
Tangazo la kuzaliwa kwa mtoto limetolewa na kuonyeshwa mbele ya lango kuu la
Kasri kuu la kifalme la Uingereza la Buckingham kama utamaduni na mila za
Uingereza zilivyo.
Taarifa rasmi iliyosainiwa na jopo la madaktari bingwa kuthibitisha
kujifungua kwa Duchess wa Cambridge ilipelekwa kwenye kasri la kifalme chini ya
ulinzi wa polisi.
Malkia wa Uingereza,Duke wa Edinburgh,Prince wa Wales, Duchess wa Cornwall na
Prince Harry pamoja na wanandugu wa familia zote wametaarifiwa juu ya kujifungua
salama kwa Kate na wote wamepokea vizuri habari hii, Imesema taarifa hiyo ya
Kasri la kifalme.
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron ameandika kwenye mtandao wa kijamii
wa Twitter ujumbe wa kuwapongeza Prince William na mkewe kwa kupata mtoto wa
kiume na kusema nchi nzima itashangilia kwa ujio wa mtoto wa kiume.
Kiongozi wa chama cha Labour Ed Miliband pia ameandika kwenye mtandao wa
kijamii wa Twitter "pongezi nyingi kwa Duke na Duchess wa Cambridge. Nawatakia
wao na mtoto wao furaha na afya njema." |
0 Comments