Karatu. Kutokana na kuwapo kwa changamoto za mabadiliko ya tabianchi, wakulima wa shayiri wameombwa kutumia na kusikiliza zaidi ushauri wa wataalamu.
Wito huo ulitolewa hivi karibuni kwenye maonyesho ya wakulima wa shayiri Kijiji cha Njiapanda getini, wilayani Karatu, mkoani Arusha.
Akizungumza na wakulima hao, Meneja wa Kiwanda cha Kuzalisha Kimea cha Moshi, Vitus Muhusi, alisema siri kubwa ya kuvuna kimea ni kufanyia kazi ushauri wa wataalamu.
Muhusi alisema wakulima wa shayiri nchini wanawezeshwa pembejeo, elimu na mafunzo bure kutoka kwa wataalamu washauri wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), hivyo wanapaswa kutumia fursa hiyo.
“Wataalamu wetu wanajua katika kipindi hiki ili mkulima aweze kupata mazao yenye tija kwa mazingira haya yenye mabadiliko ya tabianchi, anachotakiwa kufanya,” alisema Mahusi na kuongeza:

“Kwa kufuata maelezo ya watalaamu, wakulima waliofuata maelekezo walivuna kiwango kikubwa cha shayiri ya daraja la kwanza. Bila kuwasilikiza wataalamu, wakulima wataendelea kupoteza fedha bure.”

Mahusi alisema mwaka jana TBL iliokoa Dola 8 milioni za Marekani kutokana na kuzalisha takriban tani 10,300 za kimea.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Shayiri kutoka TBL, Joel Msechu, alisema hivi sasa wanapokea tani 6,000 hadi 7,00 za shayiri kutoka kwa wakulima.

Msechu alisema uchache huo unasababishwa na wakulima kulima kilimo cha mazoea, badala ya kilimo cha biashara. “Kwa mwaka huu wamelima takriban hekari 28 na wanatarajia kupata kwenye tani zaidi ya 10,000,” alisema.