Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Simai Mohamed Said (kushoto) na Mratibu wa Tume hiyo Mkoa wa Arusha na Manyara,Juma Mzalau (katikati) wakitoa ufafanuzi kwa mmoja wa wajumbe wa Baraza la Katiba wa Wilaya ya Karatu, Elibariki Dime jana wakati tume hiyo ikikusanya maoni  ya Rasimu ya Katiba Mpya. Picha na Mussa Juma. 

Wapendekeza uwe kuanzia  miaka 30 ili vijana nao wapewa nafasi kwa kuwa ndiyo wenye nguvu na uwezo kielimu.
Kibondo. Wajumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya ya Kibondo Mkoa wa Kigoma, wamesema wanataka umri wa kugombea nafasi ya rais uanzie miaka 30 ili kutoa nafasi kwa vijana kupata nafasi hiyo.

  Pia, wamesema wanataka Ibara ya 75 (d) kifungu hicho  kifutwe au kitamke kwamba sifa moja wapo ya mtu kuchaguliwa kushika nafasi ya urais itakuwa kuanzia miaka 30.

  Kwa mujibu wa mapendekezo ya Rasimu ya kwanza ya  Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji mstaafu Joseph Warioba, Ibara ya 75 (d) inasema mtu atakuwa na sifa ya kuchaguliwa kushika nafasi ya madaka ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano kama ana umri usiyopungua miaka Arobaini.Mapendekezo hayo yanakuja huku ikiwa baadhi ya wanasiasa wakiwamo Mbunge wa Kigoma Kasikazini, Zitto Kabwe na Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba waliwahi kupendekeza umri wa mtu kugombea urais uanzie miaka 30.
Umri wa Rais

Akizungumza katika mkutano wa baraza hilo, Mjumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya hiyo, Ibrahimu Juma alisema anapendekeza umri wa rais uwe miaka 30 na kuendelea.Alisema kuweka muda wa miaka 40 ni kuwanyima fursa watu wenye uwezo wa kushika nafasi ya rais, na kwamba inawanyima haki ya msingi wananchi kuwa viongozi kwani kuna vijana wengi ambao wana elimu na uwezo wa kushika nafasi hiyo.
“Kwa mujibu wa mapendekezo ya Rasimu ya Katiba Ibara ya 75 (d), inataja sifa moja ya mtu kuwa rais  ni lazima awe na umri usiopungua  miaka 40 sasa kwa maoni yangu napendekeza kifungu hicho kibadilishwe na iwe miaka 30,”alisema Juma.

  Umri wa Spika wa Bunge

 Mjumbe wa Baraza hilo, Moris Sewahana akitoa mapendekezo kwenye sura ya saba ya mapendekezo ya rasimu ya kwanza ya Katiba alisema, anapendekeza  Katiba ifute umri wa Spika wa Bunge kwani nafasi hiyo inahitaji busara na siyo umri.

  Alisema mapendekezo ya rasimu hiyo ni kwamba sifa ya mtu kumuwezesha kuwa Spika wa Bunge ni lazima awe na umri wa miaka 40 ni vyema kifungu hiko kikafutwa, kwa madai ni  kiwango cha elimu kilichotajwa kwenye rasimu inatosha kuwa sifa ya msingi.


--------------------------------------------------------
 Aidan Mhando,Mwananchi