ZIKIWA zimebaki saa chache kulishuhudia Tamasha la Matumaini 2013, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar, kesho, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe ametamba kumkalisha mpinzani wake atakayepambana naye katika ndondi, mwigizaji Vincent Kigosi ‘Ray’.ZITTO Akizungumzia pambano hilo, Zitto ambaye ni mshambuliaji katika Kikosi cha Timu ya Wabunge wa Simba alisema kuwa tayari amejiweka fiti katika kiwango cha hali ya juu ikiwa ni miezi michache tangu alipotoka kwenye mafunzo jeshini. Zitto aliapa kuwa lazima kesho ‘amtoe roho Ray’ akitamba kwamba yupo fiti baada ya kujichimbia kambini na kujiweka sawa. Alisema kuwa amepata mazoezi ya nguvu ya kurusha na kupangua ngumi na ana mbinu zote za kummaliza Ray katika raundi za mwanzo. “Nipo fiti sana, najua Ray ni mtu wa mazoezi lakini hilo halinipi shida kwa sababu na mimi nipo vizuri sana, cha msingi watu wajae Uwanja wa Taifa, siku hiyo (kesho) washuhudie nikimtoa huyo Ray roho,” alisema Zitto na kuongeza: “Ray ni mwigizaji mkubwa, ana mazoea na majukwaa ya matamasha lakini mimi nataka niwathibitishie watu kuwa naweza kumiliki ulingo vilivyo kama ninavyokuwa kwenye majukwaa ya siasa. “Kazi ni moja tu kesho (Jumapili) kwenye Uwanja wa Taifa, natoa tahadhari kuwa ‘nitamuua’ Ray. Nawaahidi watu wote ushindi ‘so’ tukusanyike tupate burudani na kuchangia elimu yetu. “Tujae tupate burudani ya aina yake, siyo burudani tu, tupeane neno la matumaini lakini pia tuchangie elimu yetu. Mkombozi wetu ni elimu hivyo tujumuike sote tuchangie elimu yetu, vijana au watoto wetu wasome katika mazingira rafiki ya kielimu.”RAY Kwa upande wake Ray ametamba kuwa yupo fiti katika kiwango chake cha juu kabisa cha mazoezi ya ndondi hivyo anachosubiri ni kukutana na mpinzani wake ammalize. Ray, katika siku za hivi karibuni amekuwa akitumia muda wake mwingi akiwa ‘gym’ ambapo ukimuona, bila kuambiwa utathibitisha kuwa yupo vizuri kimazoezi. “Zitto ni mwanasiasa machachari, najua ni mtu wa maneno mengi kwenye majukwaa ya siasa. Mimi ni mtu wa mazoezi sana na hakika Zitto hataweza kunipiga,” alisema Ray na kuongeza: “Zitto hawezi kugusa mwili wangu kwa ngumi, najua pa kupiga mpaka adondoke, ataaibika, nawaonea huruma wapigakura wake lakini watanisamehe kwa hili, nakwambia lazima akae.” Hata hivyo, Ray aliwataka mashabiki wake na watu wote kukusanyika Uwanja wa Taifa kushuhudia ngumi za kufa mtu na burudani nyingine za kila aina zinazojulikana Bongo.MASTAA WENGINE Mastaa wengine watakaonyukana ni mwigizaji Jacqueline Wolper atakayekutana uso kwa uso na Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, Aunt Ezekiel atakayevaana na Mbunge wa Viti Maalum Vijana, Mkoa wa Mara (CCM), Ester Bulaya huku Jacob Steven ‘JB’ akitaka kuzichapa na Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan.Katika ndonga za ‘maprofesheno’, Mkenya Patrick Amote atanyukana na Mtanzania Thomas Mashali huku Shadrack Muchanje wa Kenya akitoana nundu na Francis Miyeyusho wa Bongo. JK MGENI RASMI, REFA Katika tamasha hilo litakalojumuisha burudani zote nchini na neno la matumaini, mgeni rasmi atakuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete ambapo tahutubia na pia atakuwa refa wa mechi ya Wabunge wa Simba na Yanga. |
0 Comments