Dar, Moshi.
Baadhi ya abiria na watu waliokuwa wakitarajia kupokea miili ya ndugu zao waliofariki dunia nje ya nchi, walikwama kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere baada ya ndege za kutokea Kenya kusimamisha huduma kutokana na moto uliozuka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta.

Uwanja huo uliopo Nairobi ambao hutumiwa na ndege nyingi za kimataifa kuunganisha safari zake katika nchi mbalimbali, ulisimamisha kwa dharura safari za ndege zikiwamo za Shirika la Ndege ya Kenya (KQ) kwa siku nzima ya jana.

Taarifa zilisema ndege zote zilizokuwa zitue uwanja wa Jomo Kenyatta kwa siku ya jana hazikuruhusiwa, na zile zilizokuwa tayari angani zilielekezwa kutua kwenye viwanja vya ama Mombasa, Kenya au Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) uliopo mkoani Kilimanjaro, Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa, chanzo cha moto huo bado hakijajulikana, ambapo taarifa zingine zilisema kuwa moto huo ulianza kuwaka saa 11 alfajiri na kusababisha usumbufu kwa abiria na wale waliokuwa na shughuli zao kwenye uwanja huo.

Hata hivyo, vikosi vya Zimamoto na Uokoaji vilifanikiwa kuuzima. Ilielezwa kuwa moto huo ulianzia katika chumba cha Idara ya Uhamiaji kinachotumiwa na wasafiri wanaowasili.

Tukio hilo limemfanya Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta kufika uwanjani hapo kujionea hali ilivyo akiwa ameambatana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Joseph Ole Lenku na Waziri wa Usafirishaji na Miundombinu, Michael Kamau.

Kutokana na kufungwa kwa uwanja huo, marubani wamekuwa wakielekezwa kutumia viwanja vingine, ukiwamo Mombasa, Eldoret na Dar es Salaam (JNIA) na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe, Uganda.

Uwanja wa JNIA

Mmoja wa abiria, Ahmad Abdul aliyekuwa anafuatilia mwili wa jamaa yao aliyefariki dunia nchini India, alisema mwili huo ulikuwa uwasili saa tatu asubuhi kwa Ndege ya KQ, lakini tangu muda huo hadi mchana walikuwa hawajui mwili wa jamaa yao huyo utawasili uwanjani hapo muda gani.

“Mwanzoni tuliambiwa wametua Mombasa badala ya Jomo Kenyatta na jamaa zetu walikuwa hawajui mipangilio ya safari ilivyo,” alisema na kuongeza: “Baadaye tulipata taarifa ndege za KQ zimesitishwa, ikatuchanganya zaidi,” alisema Abdul.

Watendaji wa uwanja huo hawakuweza kupatikana kutokana na kudaiwa kuwapo kwenye vikao kwa muda mrefu, lakini hata hivyo, Mkuu wa Huduma ya Njia za Ndege katika Kampuni ya Kuingiza na Kupakua Mizigo Uwanjani hapo ya Swissport, Mahmood Kisukari alisema hali ya usafiri uwanjani hapo ni shwari .

Imeandikwa na Daniel Mjema Moshi, Boniface Meena, Nairobi na Joseph Zablon, Dar