Mkazi wa Zanzibar, Pili Hija akiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam jana na watoto wake walioungana.  Picha na Juliana Malondo
Dar es Salaam. 
Mkazi wa Jang’ombe Visiwani Zanzibar, Pili Hija (24), amejifungua watoto walioungana huku mmoja akiwa hana kichwa.
Watoto hao ambao wapo Wodi namba 36 katika Jengo la Wazazi la Hospitali ya Taifa Muhimbili mbali na kuzaliwa mmoja akiwa hana kichwa, wameungana sehemu ya uti wa mgongo, mkono mmoja na wanatumia njia moja ya haja kubwa.
Akizungumza na mwandishi wetu jana, mama wa watoto hao, alisema: “Nilijifungulia nyumbani, nilisikia uchungu mara moja na hapo hapo nikajifungua kwa njia ya kawaida na jirani yangu ndiye aliyenisaidia,”alisema na kuongeza:
“Nilijifungua saa moja  asubuhi, nilijua nitazaa pacha kwa kuwa nilishafanya kipimo katika Hospitali ya Makunduchi, wakaniambia nitajifungua pacha lakini mmoja si binadamu ni kiwiliwili.
“Nimeolewa, mume wangu ni mwanajeshi, nina watoto wengine wawili mmoja wa kike na mwingine wa kiume, mume wangu hajui tukio hili kwani yupo kambini Zanzibar na hatuna mawasiliano yoyote kwa sasa,” alisema.
Daktari wa Upasuaji wa Watoto Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Zaituni Bokhary alisema; “Hii ni mara ya kwanza kwa jambo hili kutokea katika miaka ya hivi karibuni. Mara ya mwisho lilitokea mwaka 1984.
“Tulikuwa tufanye upasuaji leo lakini tumeahirisha na utafanyika Alhamisi (kesho) asubuhi katika Kitengo cha Mifupa cha Muhimbili (Moi).”
Msimamizi wa Wodi ya Watoto walikolazwa, Dk Edna Majaliwa  alisema: “Hakuna sababu maalumu kitaalamu  inayosababisha watoto kuungana, mara nyingi zinapokutana mbegu za X na Y na kutengeneza mimba kunakuwa na hatua za ukuaji wiki nne, wiki nane, wiki 12, 16 na kuendelea.