Kwa mujibu wa taarifa hiyo zaidi ya wananchi milioni moja wanaishi katika eneo dogo la Goma na Sake na kandokando ya barabara ambayo inawaunganisha na kambi ya wakimbizi ya Mugungu ambayo ni makazi ya muda ya watu karibu 70,000 ambao wameyakimbia makazi yao kutokana na mapigano.
Kwa mujibu wa Monusco,tangu katikati ya Mei eneo hilo limeshuhudia mapigano ya mara kwa mara kutoka kwa Kundi la M23 dhidi ya Majeshi ya Serikali ya FARDC ikiwa ni jaribio la wazi la kutaka kusonga mbele kuelekea Goma na Sake. “Katika mashambulizi hayo,likiwamo la hivi karibuni la Julai 14, M23 walitumia kiholela silaha zao za moto zikiwamo silaha nzito ambazo zimesababisha wananchi kujeruhiwa.”
Taarifa hiyo imeongeza kwamba kundi hilo la M23 katika mashambulizi hayo limelenga pia Vituo vya Umoja wa Mataifa.
Taarifa hiyo inabainisha kwamba eneo hilo maalumu la usalama (security zone)litasaidia kudhibiti tishio la moja kwa moja mbali na eneo la nje ya Goma na pengine eneo hilo linaweza kupanuliwa na kurudiwa sehemu nyingine kutakako hitajika.
Tamko hilo la kutoa saa 48 kwa waasi kusalimisha silaha zao linafuatia kuwasili katika eneo la Goma kwa Kamanda Mkuu wa Monusco, Luteni Jenerali Carlos Alberto dos Santos Cruz ambaye alitangaza kwamba Misheni ya Monusco itaunga mkono Jeshi la Serikali(FARDC) katika kuanzisha eneo la usalama kuzunguma eneo la Goma na vitongoji vyake.
0 Comments