Stori: Makongoro Oging’ na Haruni Sanchawa
MTANDAO hatari wa unga nchini Tanzania umeshanaswa, kwa sasa unafanyiwa kazi kwa kasi na Kitengo cha Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya, chini ya kamanda wake, Godfrey Nzowa.
Habari njema kuhusu kunaswa kwa mtandao wa unga, zinakuja baada ya Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe kufanya kazi nzuri na kuwataja watu ambao inadaiwa walihusika katika kupitisha madawa ya kulevya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.Sekeseke kuu ni kukamatwa kwa Watanzania wawili, Agnes Gerald ‘Masogange’ ambaye ni mwanamitindo na Melisa Edward, nchini Afrika Kusini, wakiwa na madawa ya kulevya aina ya Crystal Methamphetamine, yenye uzito wa kg 120, Julai 5, mwaka huu.

Swali kwamba walipitaje JNIA lilijibiwa na Mwakyembe Jumamosi iliyopita, akafafanua namna Mfumo wa Kamera za Usalama (CCTV), zilivyonasa ‘uhuni’ uliofanyika, hivyo akawataja watumishi wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege (TAA), Yusuf Daniel Issa, Jackson Manyonyi, Juliana Thadei na Mohamed Kalungwana kuhusika, akaagiza wafukuzwe kazi na polisi kuwakamata.
Baada ya Mwakyembe, moto unaendelea kuwaka na uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa mtandao ulionaswa na Kitengo cha Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya, unagusa mikoa yote nchini.
Katika mtandao huo, siri kubwa iliyovuja ni majina na jinsi biashara hiyo haramu inavyoendeshwa mkoa kwa mkoa, wilayani mpaka mitaani, vilevile wanamichezo na wasanii mbalimbali ambao imeshabainika kwamba wengi wao wanatumika kusafirisha unga.
Imebainika kwamba mtandao huo, uligundulika baada ya watu 2,075 kukamatwa katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu (baadhi yao, picha zao zinaonekana ukurasa wa mbele).
“Watu tuliowakamata kimsingi ni wale wanaotumwa tu. Sasa wale ndiyo wamewataja mabosi wao, wameeleza siri kubwa,” alisema Kamanda Nzowa na kuongeza:
“Haikuwa kazi rahisi, tulitumia mbinu za kiaskari kuwafanya waeleze ukweli. Wamesimulia biashara hiyo inavyofanyika, jinsi watu wenye fedha wanavyowatumia vijana kusafirisha mizigo.
“Tulichobakiza sasa ni kuwakamata wahusika na kuusambaratisha mtandao wenyewe. Hata sasa tunachokifanya ni kupambana na huo mtandao wenyewe, mwisho tutausambaratisha kabisa.”
NI MWAKA WA VITA NZITO
Nzowa, alisema kuwa mwaka huu umeonekana kuwa na vita nzito kwa sababu kuna lindi kubwa la watu ambao wamejiingiza katika biashara ya madawa ya kulevya licha ya wengi kukamatwa na hata baadhi yao kunyongwa katika nchi za China na Pakistan.
Alisema madawa ya kulevya yenye uzito wa kilo 16,824 (tani 16.8) yamekamatwa kati ya kipindi cha Januari na Juni, mwaka huu, idadi ambayo ni kubwa kuliko vipindi vyote vilivyopita.
Alifafanua kwamba wingi huo usitafsiriwe tu kwamba biashara ya madawa ya kulevya inatanuka nchini, isipokuwa itazamwe kwa jicho la pili kwa upana wake jinsi mapambano dhidi ya biashara hiyo yalivyochochewa makali.
“Udhibiti umekuwa mkubwa sana. Isichukuliwe tu kwamba biashara inazidi kushika kasi, hapana, haya ni matunda ya kazi ya udhibiti ambayo inafanyika. Pengine huko nyuma walikuwa wanapishana kwa wingi zaidi lakini mapambano yalikuwa dhaifu, kwa hiyo wafanyabiashara hiyo haramu walikuwa wanajitanua tu.
“Ni wajibu wa kila mtu kumwambia mwenzake aachane na hii biashara, tunapomkamata na ushahidi, hapo anakuwa amekwenda na maji,” alisema Nzowa.
Akichambua zaidi, Nzowa alisema takwimu za madawa ya kulevya aina ya heroin zilizokamatwa katika kipindi hicho ni kilo 30 na washitakiwa ni 45, kati yao wanawake ni wanne.
Alisema, cocaine walikamata kilo nne na watuhumiwa ni 18 ambao ni wanaume watupu na dawa aina ya ephedrine walikamata kilo 12 mshitakiwa ni mmoja mwanaume na bangi ilikamatwa kilo 9,999 na watuhumiwa ni 1,478,  kati yao wanawake ni wawili.
Aliongeza kuwa licha ya kukamata bangi, polisi waliweza kuharibu ekari 300 za mmea huo katika mikoa ya Arusha, Tanga na Mara wilayani Tarime.
Kamanda Nzowa akaongeza kwamba polisi wanafanya kazi hiyo nzuri kwa kushirikiana na raia wema.
“Hivi sasa tuko makini sana kwa wasanii na wanamichezo wanaotaka kusafiri kwenda nje ya nchi kwa sababu tumegundua kuwa wanatumika kutokana na umaarufu wao,” alisema Nzowa.
Akifafanua zaidi, kamanda huyo alisema wana taarifa kwamba hivi sasa kuna dawa za kulevya za majimaji, hivyo wanaofikiria kusafirisha hizo kwa njia hiyo wanapaswa kujua kuwa watagundulika.
“Hii ni vita ambayo kila anayelitakia mema taifa hili anapaswa kushiriki kupambana na dawa za kulevya,” alisema Kamanda Nzowa.
KWA NINI VIJANA WENGI WANAKIMBILIA UNGA?
Mtafiti maarufu na mwelimishaji wa maisha ya vijana na jamii kwa jumla, James Mwang’amba, alisema kuwa vijana wengi wanaingia katika wimbi la biashara ya madawa ya kulevya kwa sababu ya kukata tamaa.
“Ukifuatilia maisha ya vijana kwa sasa, utagundua kwamba wengi wao wamekata tamaa. Wanahisi hawana njia ya kutoka kimaisha ndiyo maana wanaona fursa yoyote inayokuja mbele yao inafaa hata kama ni hatari.
“Kila mtu anatamani sana maisha ya juu, awe na kipato kikubwa, sasa kwa vile haoni njia nzuri za kufikia ndoto zake, anaamua kujiingiza kwenye usafirishaji wa madawa ya kulevya ili apate fedha za haraka ili naye awe mtu fulani,” alisema Mwang’amba na kuongeza:
“Tatizo kubwa ni hii tofauti ya kipato. Kuna tofauti kubwa sana kati ya wenye nacho na wasio nacho, hii ni hatari sana. Sasa jamii kwa vijana ni hatari zaidi kwa sababu damu inachemka na kuona kila kitu ni rahisi kufanya.
“Hakuna sababu nyingine kwa nini vijana wengi wanakuwa wauza unga, ukweli ni tamaa ambayo inachochewa na hasira ya kuwa na maisha duni wakati wanawaona wengine wakiwa matajiri wakubwa.”