Na Khatimu Naheka
HATIMAYE Yanga imefanikiwa kuinasa saini ya kiungo raia wa Uganda, Moses Oloya (pichani), baada ya kumsainisha mkataba wa miaka miwili, jana jijini Dar es Salaam.
Oloya awali alikuwa akiwaniwa na Simba waliotangulia kuanza mazungumzo na nyota huyo, lakini ilishindikana kutokana na kuwa na mkataba na Klabu ya Saigon Xuan Thanh ya Vietnam.
Taarifa za kuaminika zilizolifikia Championi Ijumaa, zimesema kuwa Oloya alitua jijini Dar es Salaam, juzi usiku kwa siri, majira ya saa nne akitokea Vietnam kupitia nchini Kenya, ambapo mara baada ya kutua alipelekwa moja kwa moja katika hoteli moja kubwa jijini (jina tunalo) na kufichwa humo.
Baada ya kufika hotelini hapo, wahusika walipewa maelekezo kuwa hawatakiwi kutoa taarifa zozote juu ya mchezaji huyo ambaye alikuwa akisubiri kusaini.
Jana mchana, alikutana na viongozi wanne wa juu wa Yanga, ambao walizungumza kwa kirefu na nyota huyo, mwisho wakakubaliana kila kitu juu ya mkataba ambapo Oloya alisaini mkataba wa miaka miwili ulioigharimu klabu hiyo zaidi ya dola 74,000 (Sh milioni 120).
“Kila kitu tumekuwa tukikifanya kwa siri kubwa, hatukutaka kuanza kuzungumza kama wanavyofanya wenzetu (Simba), tulikuwa na uhakika kuwa huyu mchezaji (Oloya) tutamleta hapa Yanga, tunashukuru hilo kukamilika, sasa tutakwenda kumalizia vitu vidogo sana,” alisema kiongozi mmoja wa Yanga na kuongeza:
“Tumelazimika kufanya hivi kwa kuwa tulitaka kila kitu kimalizike kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili, sasa tunageuka katika kazi ndogo iliyosalia ya kumalizana na klabu yake ambayo amebakiza muda wa wiki zisizozidi tatu katika mkataba wake.”
Kufuatia kukamilika kwa usajili huo, nyota huyo aliondoka jana usiku akiongozana na mmoja wa mabosi wa klabu hiyo (jina tunalo) tayari kwenda kumalizana na klabu yake ya nchini Vietnam kabla ya kurudi kuja kuitumikia Yanga.
Gazeti hili lilikuwa la kwanza kuandika juu ya Yanga kufanya mazungumzo na Oloya, baada ya Simba kusema kuwa inamuwania Mganda huyo.