Wanafunzi wa moja ya shule zilizopo katika Wilayani Bukombe, kama walivyokutwa na mpigapicha wetu
Bukombe: Wakati Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ikizindua Mpango wa Kuleta Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now) katika Sekta ya Elimu Tanzania leo, maelfu ya watoto wenye umri wa kwenda shule katika vitongoji kadhaa vya Kijiji cha Namalandula, mkoani Geita wanasoma katika mazingira duni kutokana na shule walizozianzisha kutosajiliwa hadi sasa.
Waziri wa Elimu, Dk Shukuru Kawambwa ndiye atakayezindua mpango huo leo sambamba na maonyesho yenye lengo la kuelimisha na kupata maoni ya wadau katika utekelezaji wa vipaumbele vya sekta ya elimu.
Wakati hayo yakiedelea, katika vitongoji vya Ilyamchele na Mutukula vilivyopo Wilaya ya Bukombe zimejengwa shule za msingi ambazo kwa muda wote wa uhai wake unaokaribia miaka 10, zimekuwa zikitoa ‘elimu ya awali’ tu, licha ya kwamba zina madarasa kadhaa.Maisha ya kielimu katika shule hizi ni ya kuhuzunisha kutokana na kwamba hazijasajiliwa hali ambayo ina athari kubwa kwa maelfu ya watoto wanaosoma hapo sasa na wale ambao wamewahi kusoma hapo.
Mazingira ya shule zote mbili ni duni na hazina miundombinu kwani madarasa yamejengwa kwa miti na baadhi yake yameezekwa kwa nyasi. Idadi kubwa ya watoto inawafanya walimu wa kujitolea katika shule hizi kuchanganya madarasa.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji (VEO) cha Namalandula, Jackson Bwire anasema shule hizo zilianzishwa na wananchi kutokana na kutokuwapo kwa huduma za elimu katika maeneo yao ambayo yana kaya zaidi ya 3,500 hivi sasa, zenye watoto wapatao 7,000 na kwamba nusu yao wanapaswa kuwapo shuleni wakisoma.Mwananchi lilishuhudia katika Shule ya Ilyamchele wanafunzi wakisoma kwa zamu (wengine asubuhi na wengine mchana) wakati katika Shule ya Mutukula, darasa la kwanza wanasoma peke yao kutokana na wingi wao wakati darasa la pili wanachangamana na la tatu na darasa la nne wanachanganyika na darasa la tano.
Awali wanafunzi katika shule hizo walikuwa wakisoma mpaka ‘darasa la sita’ lakini sasa wengi wanaishia darasa la nne, kisha kupelekwa katika Shule ya Msingi ya Namalandula ambako hufanya mtihani wa darasa la nne na wenzao kwa lengo la kuendelea na darasa la tano baadaye.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji (VEO) cha Namalandula, Jackson Bwire aliliambia gazeti kuwa baadhi ya watoto ambao walifaulu darasa nne wameshindwa kuendelea darasa la tano kutokana na umbali uliopo kutoka katika vitongoji wanakotoka na ilipo shule iliyosajiliwa.
Hivi sasa shule hizi kwa pamoja zina wanafunzi 954; Ilyamchele ambayo pia inajulikana kama Kashishi ikiwa na wanafunzi 600 na walimu watatu wakati shule ya Mutukula ina wanafunzi 354 na walimu watano.
Mwezi Mei mwaka huu Shule ya Ilyamchele ambayo ilianzishwa mwaka 2004 ilikuwa na na wanafunzi 783; wavulana 402 na wasichana 381 wakati Shule ya Mutukula ambayo ilianzishwa 2008, ilikuwa na wanafunzi 410; wavulana 183 na wasichana 327.Baadhi ya walimu wa shule hizi wanasema kupungua kwa idadi ya watoto kulitokea baada ya shule hizo kufungwa kwa muda na ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe kabla ya kufunguliwa baadaye kwa maelekezo ya Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Geita, Joseph Musukuma.
Watoto wote hawa majaliwa yao kielimu hayajulikani kutokana na shule hizi kutokusajiliwa hadi sasa, hivyo hata kama wangehitimu wakiwa na uwezo wa kufanya mtihani wa Darasa la Saba hawawezi kupata fursa ya kujiunga na sekondari wala chuo chochote nchini. Shule zao hazitambuliki kwa mujibu wa sheria za nchi.
Walimu wanafundisha katika shule hizi ni wa kujitolea lakini hawana taaluma ya ualimu. Baadhi yao wana elimu ya darasa la saba na wengine kidato cha nne na malipo yao ni kila mmoja kupewa shamba la ekari sita ili aendeshe shughuli za kilimo.Baadhi ya wakazi wa vitongoji hivi viwili waliozungumza na gazeti hili lilipotembelea vijiji hivyo walisema waliamua kuanzisha shule hizo ili kuwasaidia watoto wao ambao hawakuwa wakisoma kutokana na Shule ya Msingi ya Namalandula kuwa mbali.
“Kama mtoto akitoka hapa kwenda Namalandula kusoma inabidi atembee kwa masaa mawili na nusu au matatu, halafu anapita kwenye pori, kweli hapo unaona inawezekana?,”alihoji Elizabethi Leonard, ambaye ni mkazi wa Kitongoji cha Mutukula.Mazingira ya shule
Mbali na madarasa ya shule hiyo kuendeshwa katika majengo yasiyokuwa na sifa hiyo (vibanda vya miti na nyasi), hakuna viti wala madawati na watoto wanakaa chini na wengine juu ya mawe.
Kadhalika katika vibanda hivi ndiko walimu wametenga nafasi ambazo wamekuwa wakizitumia kama ofisi za kuendeshea shughuli zao. Walimu wanatumia ubao wa sataranji (ceiling board) kuandikia na mara nyingi baada ya kufundisha watoto hutoka na ubao huo nje na kuegesha kwenye mti kwa ajili ya kunukuu yaliyoandikwa.
Kiongozi wa walimu katika Shule ya Ilyamchele, Sanane Kalidushi anasema kutokana na wingi wa watoto wanaohitaji huduma ya elimu, wanalazimika kuwaingiza kwa zamu madarasani. “Tupo watatu tu na tunajitahidi hivyohivyo maana wanafunzi ni wengi,” anasema Kalidushi ambaye hvi sasa shule yake hiyo ina wanafunzi 600.
Kwa upande wa shule ya Mutukula hali ni tofauti kwani Kiongozi wake, Alphonce Lubinza anasema watoto huchanganywa kwenye madarasa. “Tunawachanganya kwa hiyo mwalimu akiingia kufundisha darasa la pili, darasa la tatu inabidi wasiandike maana somo haliwahusu,” anasema Lubinza.
Alipoulizwa kwa nini wanafunzi hao wasiingize kwa zamu madarasani, Lubinza alijibu: “Tunaogopa kwa sababu ukiwaruhusu wakae nje kwa muda mrefu wanatoroka na kurejea nyumbani”.
Kuhusu vifaa vya kufundishia kama vile vitabu, walimu katika shule zote mbili walisema wanaazima kutoka Shule ya Namalandula na kisha huvirejesha pale vinapohitajika.“Huwa wanatuazima kwa muda kama wa miezi mitatu na huwa tunavirudisha kama vile kwa ukaguzi na wakiridhika kwamba viko katika hali nzuri basi hutuazima tena,” alisema Kalidushi.
Katika Shule ya Mutukula, gazeti hili lilishuhudia idadi kubwa ya watoto wa darasa la nne wakiwa wamezunguka kitabu kimoja ambacho walipewa na mwalimu wao kunukuu baadhi ya maswali kwa lengo la kuyajibu.
Msimamo wa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe ni kwamba shule hiyo ifungwe kwani haistahili kutoa elimu kutokana na kutokuwa na vigezo husika.
Ofisa Elimu ya Msingi katika wilaya hiyo, Shadrack Kabanga akizungumza kwa simu alisema yeye anachokifahamu ni kwamba shule hizo zilishafungwa na hana taarifa kama zinaendelea.“Mimi najua hizo shule tulizifunga baada ya kubaini hazijasajiliwa na hazina vigezo vya kuitwa shule, nashangaa kusikia zimefunguliwa na zinazoendelea na mafunzo,” alisema Kabanga.
Hata hivyo, alipotakiwa kuzungumzia mpango wa kuboresha elimu kwa watoto vitongoji hivyo ambavyo vina idadi kubwa ya watoto wanaotakiwa kwenda shule na hakuna shule katika maeneo hayo, Kamanga alikataa kusema chochote na kutaka atafutwe mkurugenzi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bukombe, Liliani Matinga alipoulizwa kuhusu shule hizo alisema hawezi kuzungumzia suala hilo na badala yake alitaka atafutwe Ofisa wa Elimu ya Msingi wa halmashauri hiyo.Msimamo wa kuzifunga shule hizo unapingwa na wananchi ambao wanasema, “Lazima watoto wetu wafute ujinga walau wa kutojua kusoma na kuandika.”
Diwani wa Kata ya Namonge ambayo pia inasimamia Kijiji cha Namalandula, Patrick Kalugusi anakiri kwamba shule hizo hazijasajiliwa na kwamba jitihada za ujenzi wa madarasa zinaendelea ili kuziwezesha kupata kibali.
Kauli yake inafanana na ile iliyotolewa na Bwire ambaye ni VEO wa Namalandula akisema kuwa katika shule zote mbili tayari wananchi wameanza ujenzi wa maboma kwa madarasa mawili ikiwa ni hatua ya kuwezesha shule hiz o kusajiliwa.
|
0 Comments