Ni vigumu kuzungumzia historia ya Lugha ya Kiswahili nchini ukaeleweka na wapenda lugha hiyo duniani bila kumtaja marehemu Shaaban Robert, kutokana na ukweli kuwa amekuwa mshairi na nguli katika lugha hiyo.
Mchango wa Shaaban Robert katika lugha ya Kiswahili una thamani kubwa kutokana na riwaya na mashairi yaliyojaa mafunzo na hekima kubwa jambo ambalo limempa heshima na kusababisha azidi kukumbukwa kila muda unavyozidi kusonga mbele.
Jina la Shaaban Robert linafahamika vyema ndani na nje ya mipaka ya Tanzania na kusababisha kazi za vitabu vyake kutumika shuleni pamoja na vyuo vya kati na vya juu nchini na kwingineko Duniani.
Aisha Jafary, mtoto wa kaka yake Shaaban Robert akiwa na mwanaye, MwanaAkida Jafary (kushoto). Picha na Burhani Yakub 
aba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika uhai wake akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizithamini na baadaye kuzitangaza kazi za marehemu Shaaban Robert hadi kufikia kuziingiza katika kumbukumbu ya historia ya Taifa la Tanzania.
Hata barabara ya kwenda Ikulu inaitwa jina lake ‘Barabara ya Shaaban Robert’
Barabara kuu ya kuingia  Ikulu ya Dar es Salaam kupitia Jumba la Makumbusho imepewa jina la Shaaban Robert. Barabara hii ni sehemu tu ya maeneo ikiwamo mitaa ya Jiji la Dar es Salaam na mikoa mingine iliyopewa jina la kumuenzi gwiji huyu.
Shaaban Robert alizaliwa siku ya mkesha wa mwaka mpya mwaka 1909 katika Kitongoji cha Vibambani, Kijiji cha Machui ambacho kipo umbali wa kilomita 10 Kusini kutoka Tanga mjini.
Wazazi wake Shaaban Robert asili yao ni Kabila la Wahiyao, waliotokea  mikoa ya Kusini mwa Tanzania sehemu za katikati ya Lindi na Mtwara iliyokuwa imebobea katika desturi na mila za Uswahili.
Simulizi zinaonyesha upo mkanganyiko kuhusiana na ni namna gani baba yake aliitwa jina la Robert wakati historia inaonyesha Shaaban Robert alizaliwa katika kile kinachoelezwa kuwa ni ukoo wa Waswahili na Waislamu halisi. Shaaban ni jina la Kiislamu, Robert ni la Kikristo.
Mwandishi wa makala haya anasema wakati anafuatilia juu ya mtu huyu, alizungumza na baadhi ya ndugu zake Shaaban Robert, hakuna aliyekuwa tayari kuweka wazi juu ya jina hili na baba yake yaani Robert.
Mmoja wa watoto wake ambaye pia amefuata nyayo za baba yake za umahiri wa utunzi wa mashairi na uandishi wa riwaya, Ikbar Shaaban Robert anasema pamoja na kufuatilia sana hajapata siri hasa ya jina hilo la Robert kupewa babu yake.
Simulizi nyingine zinaeleza kuwa Robert lilikuwa ni jina halisi la baba yake Shaaban Robert lakini simulizi nyingine zinakataa na kueleza halikuwa jina la baba yake mzazi, bali alipewa tu kutokana na yeye mwenyewe kulipenda.Elimu yake aliipata katika Shule ya Msimbazi jijini Dar es Salaam kati ya mwaka 1922 na 1926, alifanya vizuri shuleni katika masomo yake na kupata cheti za kuhitimu masomo.
Alianza kazi mwaka 1926  akiwa Karani katika Idara ya Forodha ya Serikali ya Waingereza na alipangiwa kazi ya kusimamia shughuli mbalimbali katika Bandari ya Pangani mjini, Pangani Mkoa wa Tanga.
Kwa miaka miwili kati ya mwaka 1944 na 1946, alifanya kazi katika Idara ya wanyamapori na mwaka 1946 hadi 1952 akahamishiwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga na baadaye akahamishiwa  idara ya Mipango hapohapo mkoani.
Shaaban Robert alijiunga uanachama wa Kamati ya Kiswahili Afrika Mashariki (East Africa Swahili Committee), Taasisi ya Fasihi ya Afrika Mashariki (East Africa Literature Bureau) na Bodi ya Lugha Tanzania.
Tuzo kutoka kwa Malkia
Katika kuenzi kazi zake za kukiendeleza na kukikuza Kiswahili, Shaaban Robert amewahi kupata tuzo mbalimbali ikiwamo ile ijulikanayo kama ‘The Margaret Wrong Memorial Prize’.
Tuzo nyingine ni ile ya Member of British Empire MBE  na ile ya Malkia wa Uingereza (By Her Highness The Queen of England)
Kwa idadi, Marehemu Shaaban Robert katika uhai wake aliwahi kutunga hadithi nyingi lakini alizoandika jumla yake ni  vitabu 22 vya hadithi fupi, mashairi na insha. Baadhi ya kazi hizi zinatumika kufundishia katika madarasa ya shule mbalimbali ndani na nje ya nchi, vingine vimetafsiriwa katika lugha za Kiingereza, Kirusi, Kichina na Kijerumani.
Shaaban Robert alifariki Juni 22, 1962 akiwa na umri wa miaka 53 na kuzikwa katika Kijiji  cha Machui, Kitongoji cha Vibambani.
Mtu huyu bado anakumbukwa kama ni hazina kwa Taifa la Tanzania na ni tunu ya Mkoa wa Tanga kwani mbali ya kuzaliwa Tanga, karibu maisha yake yote ya kitumishi serikalini aliyatumia akiwa katika ardhi ya Tanga akiwa wilayani Pangani na Tanga Mjini.
Mchango wa Shaaban Robert katika lugha ya kiswahili ni mkubwa hasa katika uhamasishaji jamii ya ndani na nje ya Tanzania kupenda kuizungumza na kuiandika kwa njia ya mashairi, tenzi na riwaya kwani kazi zake zimefika mbali.
Huwezi kuhitimu Kiswahili bila kusoma kazi za Shaaban Robert