Arusha. 
Huku dola ikiahidi kuwakamata watuhumiwa, mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite, Erasto Msuya (43) jana alizikwa huko Kairo, Mirerani, Simanjiro katika mazishi yaliyohudhuriwa na watu wengi wakiwamo vigogo wa Serikali.
Miongoni mwa vigogo waliohudhuria mazishi hayo ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Steven Maselle ambaye aliwasilisha salamu za rambirambi za Rais Jakaya Kikwete. Wengine waliokuwapo ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka na Naibu Kamishna wa Polisi, Lazaro Mambosasa, ambaye alimwakilisha Mkuu wa jeshi hilo, IGP Said Mwema.
Katika mazishi hayo yaliyokuwa na watu wengi kiasi cha Kamati ya Mazishi kulazimika kusitisha utoaji wa heshima za mwisho, Mulongo alisema wauaji wa Msuya watasakwa na kufikishwa mahakamani wiki ijayo.“Waliomuua Msuya wataumbuka mchana kweupe wiki ijayo watakapofikishwa mahakamani. Nawahakikishia kuwa vyombo vya dola viko kazini na ukweli kuhusu waliohusika na tukio hili la kinyama utajulikana hadharani wiki ijayo wahusika watakapofikishwa mahakamani,” alisema Mulongo katika ibada ya mazishi iliyoongozwa na Askofu wa KKKT la Dayosisi ya Meru, Paul Akyoo.
Mambosasa alisema IGP Mwema amewaagiza polisi katika mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro kuwasaka na kuwafikisha mahakamani wahusika wote bila kujali majina, ukwasi wala vyeo vyao.Maselle alisema Rais Kikwete ameshtushwa na kusikitishwa na mauaji ya Msuya aliyekuwa mfanyabiashara maarufu katika mikoa ya Arusha, Manyara, Tanga na Kilimanjaro.
Aliwataka wote walioguswa na kifo hicho kuwa na subira na uvumilivu kwa kuondokewa na mpendwa wao huku akiahidi kuwa vyombo vya dola vitafanya uchunguzi na upelelezi wa kina kuhakikisha wahusika wanatiwa mbaroni na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Askofu Akyoo alikemea utajiri wa dhuluma na kafara.
Katika mahubiri yake yaliyochukua dakika 30, alisema utajiri wa aina hiyo hauna baraka wala amani kwa wahusika kutokana na dhamira zao kuwasuta kila wanapokumbuka uhalifu walioutenda.
Mwili wa Msuya ulifikishwa Kairo saa nne asubuhi kutoka Arusha kwa msafara wa magari ya kifahari zaidi ya 150 pamoja na mabasi madogo 10 yaliyobeba waombolezaji.
Msuya aliyeuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana Agosti 7, mwaka huu, aliteremshwa kaburini saa 10:20 jioni.