Dar es Salaam.
Siku tano baada ya raia wawili wa Uingereza kumwagiwa tindikali visiwani Zanzibar, Serikali kupitia vyombo vyake vya uchunguzi imeibuka na kueleza kuwa bila wananchi kutoa taarifa za ushahidi wa uhalifu wa aina mbalimbali, ni vigumu kuwabaini wahusika.
Kauli hiyo ilitolewa kwa pamoja jana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema, Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) Eliezer Feleshi, katika mkutano wao na waandishi wa habari, uliolenga kueleza mikakati ya kupambana na matumizi yasiyo sahihi ya tindikali nchini.
Katika ufafanuzi wao walisema, “Kutoa taarifa ya uhalifu wa jambo lolote siyo hiari, ni jukumu la kisheria na kikatiba,” huku Feleshi akitolea mfano jinsi Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk Steven Ulimboka alivyoshindwa kutoa ushahidi wa tukio lililomkuta la kutekwa, kupigwa na kisha kutupwa katika Msitu wa Mabwepande, hivyo kufanya uchunguzi kuwa mgumu.
Agosti 7, mwaka huu raia wawili wa Uingereza, Kate Gee (18) na Kirstie Trup (18) walimwagiwa tindikali katika maeneo ya Mji Mkongwe, Zanzibar na vijana wawili waliokuwa wakiendesha pikipiki aina ya Vespa, Waingereza hao wa walisafirishwa siku tatu zilizopita kurudi kwao kwa ajili ya matibabu.

Kuhusu polisi inavyopambana na uhalifu huo aliouita kuwa ni ‘Uhalifu mpya nchini’, IGP Mwema alisema:
“Mkemia Mkuu, Polisi hawawezi kubaini matukio haya bila ushirikiano wa wananchi kwani Tanzania ni nchi kubwa na ina watu zaidi ya milioni 45. Watu wanaingiza tindikali lakini wapo ambao wanatumia tindikali hiyo kwa matumizi haramu.”

Alisema tindikali inaweza kutolewa kwa ajili ya shughuli za viwandani, maabara na usafirishaji na kwamba watu wanapotaka kuitumia kwa ajili ya kufanya uovu wanaweza kugundulika kupitia kwa taarifa zitakazotolewa na wananchi, kwa sababu wanakuwa wamezungukwa na jamii ya watu mbalimbali.

“Kama wanataka kuitumia tindikali kwa ajili ya matumizi mabaya wananchi wanaweza kugundua kwa sababu wanakuwa wanaishi karibu na watu hao, mwananchi mwema anaweza kuwa chanzo kizuri cha kuweza kuzuia na kutoa taarifa za kuwabaini wahusika,” alisema Mwema.

Alisema wananchi wanatakiwa kutambua kuwa shughuli za kibiashara za kuwawezesha kupata kipato cha kila siku hazitafanikiwa kama hakutakuwa na ustawi wa amani.

“Tishio la tindikali linaweza kutia hofu na taharuki katika jamii, hatutaki jambo hili liendelee nchini, tunaamini wazi kuwa hakuna mtu anayeweza kufanya uhalifu akawa peke yake bila kujulikana na mtu hata mmoja,” alisema na kuongeza:

“Tunaweza kubaini kupitia kwa mhusika (mwathirika), mhalifu mwenyewe (anayetenda tendo husika) na mazingira yaliyowezesha mtu ammwagie mwingine tindikali, tukitumia nafasi hizo vizuri, moja kati ya vyanzo hivyo vinaweza kutusaidia kutambua wahusika.”

chanzo cha habari