Mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, kuhusu Rais kuwateua Wakuu wa Majeshi Nchini, yamezua mvutano kwa Wajumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya ya Liwale, Mkoani humo, wakipinga mapendekezo hayo na wengine wakiyaridhia.
Hayo yalijitokeza juzi wakati wa mkutano wa kuijadili Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba Mpya na wajumbe hao kueleza kuwa Rais kuwateua wakuu wa majeshi hawatatenda haki dhidi yake.
Baadhi walieleza Rais ni Mkuu wa Nchi hivyo jukumu hilo kutokufanywa na yeye ni kuhatarisha usalama wa taifa na wakati wowote nchi inaweza kupinduliwa. Akiwasilisha maoni ya kundi la tatu, Juma Mangora alisema Mkuu wa Majeshi asiteuliwe na Rais, bali jukumu hilo lifanywe na Baraza la Taifa la Ulinzi.
“Kama Mkuu wa Majeshi atateuliwa na Rais kutakuwa na kila hila ya kulipa fadhila na inakuwa vigumu kumchukulia hatua kali pindi atakapokiuka taratibu kutokana na kujuana zaidi,” alisema Mangora na kuongeza: “Ili kuleta uwajibikaji wa Jeshi hilo, Baraza la Taifa la Ulinzi likichukua jukumu hilo litamfanya hata Mkuu huyo wa jeshi kutokumwogopa Rais na kutekeleza majukumu yake ipasavyo.”
Naye Mohamed Dondwa alisema Mkuu wa Jeshi la Polisi anatakiwa kupatikana kupitia Baraza la Wakuu wa Polisi kutokana na wao kumjua yupi anayestahili. Alisema kumpata Mkuu wa Polisi kupitia kuteuliwa na Rais hakutakuwa na utendaji uliotukuka miongozi mwa jeshi hilo na wananchi kuendelea kulilalamikia kutokana na kutokutenda haki kila kukicha.Kwa upande wake, Hashim Majanjagara alisema kuwapata wakuu wa majeshi pasipo Rais kuhusika kuwateuwa nchi inaweza kupindiliwa pasipo kujua. “Rais ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama hivyo yeye ndiye anatakiwa kuwateuwa bila kufanya hivyo na kutumia njia nyingine wanaweza kumsaliti kwa kushawishiwa na baadhi ya watu nan chi kuingia katika hatari na vita,” alisema Majanjagara.
Wajumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya ya Liwale, mkoani Lindi, wamevutana kuhusu uwepo wa nafasi ya mgombea huru katika Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, wakieleza kuongeza wigo wa kukithiri vitendo vya rushwa. Mjumbe wa Baraza hilo, Anord Ligai akiwasilisha maoni ya kundi la kwanza alisema, kuwapo kwa mgombea binafsi kutasababisha kupata kiongozi asiyekuwa na uadilifu kutokana na kutokupitia michakato ya kumpata. Abasi Matulilo alisema, katika mambo saba ya Muungano moja wapo ni vyama vya siasa hivyo kuwapo kwa mgombea huru kutaligawa taifa.
Na Ibrahim Yamola, Mwananchi
|
0 Comments