WAKATI Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Robert Manumba wakielekea kumaliza muda wao wa kuliongoza jeshi hilo Desemba 31 mwaka huu, tayari majina sita ya maofisa wa juu wa jeshi hilo yameanza kutajwa kurithi nafasi hizo, MTANZANIA Jumapili limedokezwa. Gazeti hili limedokezwa majina manne ya maofisa wa ngazi za juu wa polisi ambao wanapewa nafasi kubwa ya kurithi kiti cha Mwema, kutokana na sifa na uzoefu wa uchapakazi wao.
Wanaotajwa kurithi nafasi ya Manumba ni maofisa wawili wa ngazi za juu wa Jeshi hilo, nao wakitajwa kuwa na sifa na uzoefu wa kiti hicho.
Kwa upande wa nafasi ya IGP, wanaotajwa ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwan Othuman, Mkuu wa Utawala na Rasilimali Watu Thobius Andengenye na Kamishina wa Operesheni wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja.
Hata hivyo gazeti hili limedokezwa kuwa katika orodha hiyo, Chagonja ndiye anapewa nafasi ndogo ya kurithi kiti hicho cha Mwema, kutokana na kile kinachodaiwa kuwa amekuwa akiandamwa na kashfa mbalimbali za kiutendaji ndani ya nje ya Jeshi hilo.
Pia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Mangu pamoja na kutajwa kuwa na sifa nyingine naye anatajwa kupewa nafasi ndogo ya kuteuliwa kwa sababu ya madai ya ukabila.
Kwa upande wa nafasi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), wanaotajwa ni ACP Advocate Nyombi, ambaye yupo Ofisi ya Upelelezi Makao Makuu kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela.
Nyombi anapewa nafasi kubwa ya kurithi nafasi hiyo kwa kile kinachoelezwa kuwa licha ya uchapaji kazi wake na kuonyesha uaminifu kwa viongozi wake, pia amekuwa na mahusiano mazuri na viongozi wake karibu wote.
Kenyela, ambaye kwa sasa amehamishiwa Makao Makuu ya Jeshi hilo akitumikia kitengo cha Upelelezi na Makosa ya Jinai, jina lake lilianza kutajwatajwa mara tu alipoondolewa Kinondoni na kuhamishiwa Makao Makuu.
Kutajwa kwa Kenyela kunatokana na kile kinachodaiwa kuwa ni rekodi safi aliyoiacha Kinondoni, kwamba hakuwa na kashfa nyingi ukilinganisha na makamanda wengine waliopitia hapo.
Manumba ambaye hakuongezewa muda na hivyo kulazimika kustaafu Desemba 31 mwaka huu sambamba na IGP Mwema, hata hivyo nafasi yake hiyo inaangaliwa kwa makini kwa sababu ni moja kati ya maeneo nyeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani.
Hata hivyo pamoja na majina hayo kuanza kutajwatajwa, hatma ya watu watakaorithi nafasi hizo inabaki mikononi mwa IGP mwenyewe pamoja na Rais Jakaya Kikwete.
Gazeti hili limedokezwa kuwa taratibu za kuwapata warithi wa nafasi hizo zinaanzia kwa IGP aliyepo madarakani ambaye anaweza kutumia njia mbili kupendekeza majina ya maofisa ambao anaona wanafaa kurithi kiti chake na kisha kuyapeleka kwa rais kwa ajili ya uteuzi.
Kwamba IGP ana nafasi kubwa ya yeye mwenyewe kuamua kupendekeza majina hayo na kuyapeleka moja kwa moja kwa rais au kuamua kutumia njia ya pili ambayo ni kuunda kamisheni ndogo itayowashirikisha watu wake wa karibu, akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye kwa sasa ni Emmanuel Nchimbi.
Ofisa wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi aliliambia gazeti hili kuwa chini ya kamisheni hiyo, majina yatapendekezwa na kupelekwa kwa rais kwa ajili ya uteuzi.
“Kuhusu mchakato kuna mambo matatu yanaweza kufanywa, kwanza IGP mwenyewe anaweza akapendekeza majina na kupeleka kwa Rais. Pili IGP anaweza akateua baraza dogo la watu wake wa karibu na kufanya uteuzi wa majina ambayo atayapeleka kwa Rais ili achague IGP mpya au IGP anaweza kukaa pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani kwa ajili ya kupendekeza majina na kupeleka kwa Rais kwa ajili ya uteuzi,” alisema Ofisa huyo wa Jeshi la Polisi.
Kuondoka kwa IGP Mwema (60) Desemba mwaka huu kumekuja baada ya kukataa kusaini mkataba wa miaka miwili ambao ungemuweka madarakani hadi mwisho wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi kimesema kuwa IGP Mwema, amekubali kuendelea kutumikia nafasi hiyo kwa miezi sita tu.
“Ninachojua mrithi wa nafasi hiyo ameishapatikana japokuwa kwa sasa ni siri kati ya IGP Mwema na bosi wake, Rais Kikwete, ila Mwema yeye naona ataondoka tu, wenzake kama Kamanda Suleiman Kova na Isaya Mngullu hawa waliongezewa muda na wamekubali,” kilisema chanzo hicho.
IGP Mwema alitakiwa kustaafu mwezi uliopita, lakini amelazimika kutii ombi la serikali lililomtaka walau aendelee kwa miezi sita baada ya yeye kukataa mkataba wa miaka miwili.
Zipo taarifa zinazodai kuwa sababu kubwa inayomfanya IGP Mwema kukataa mkataba mrefu wa kukitumikia cheo chake ni kuchoshwa na matukio mbalimbali ambayo yanaliandama Jeshi la Polisi, lakini pia mahusiano ya mashaka yaliyopo baina yake na viongozi wengine.
Kabla ya kuteulikwa kuwa IGP, Said Mwema alikuwa mtumishi Jeshi la Polisi la Kimataifa lisilokuwa na mipaka (Interpol) jijini Nairobi.
Mwaka 2006, Rais Jakaya Kikwete, alimpa ruhusa IGP Mwema kufanya mabadiliko makubwa katika Jeshi la Polisi nchini ambalo lilikuwa limepakwa matope ya rushwa na tuhuma mbalimbali za uchafu.
Inaelezwa kuwa pamoja na changamoto nyingine, lakini moja ya mafanikio makubwa aliyofikia katika uongozi wake ni kuliweka jeshi hilo karibu na wananchi kwa kuanzisha mfumo wa polisi jamii ambao umesaidia kudhibiti matukio mbalimbali ya uhalifu, ukiwamo ujambazi sugu.
Hata hivyo IGP Mwema katika uongozi wake amekumbana na changamoto mbalimbali, hasa za kisiasa ambazo zimesababisha shutuma za uvunjifu wa haki za binadamu, yakiwamo mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.
0 Comments