Mkurugenzi Mtendaji wa MNH,Dk Marina Njelekela anasema kutokana na kupatikana kwa mtambo huo wa kisasa hospitalini hapo, wanaiomba serikali iwape fedha hasa zile ambazo imekuwa ikitumia kuwasafirisha, kuwatibu wagonjwa wa moyo hasa nchini India na kwingineko.
Badala yake, MNH inaomba fedha hizo ziwasilishwe hospitalini hapo ili wagonjwa wengi zaidi waweze kutibiwa nchini. Anasema mtambo huo unaojulikana kwa jina la Catherization Laboratory, ndiyo mtambo ambao wagonjwa wengi nchini walikuwa wakisafirishwa nje kwenda nchini India kwa ajili ya matibabu.
“Sambamba na asilimia 70, pia serikali itapunguza gharama ya dola za Marekani 10,000 kwa kulipia matibabu ya mgonjwa mmoja anaetibiwa nje ya nchi ukilinganisha na Dola 6,000 kwa matibabu ya hapa nchini.
“Kupitia uwepo wa kituo hicho hapa Muhimbili, uongozi wa hospitali upo katika mazungumzo na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ili kulipia kiasi cha dola za Marekani 6,000 badala ya dola 10,000 kwa gharama ya mgonjwa mmoja anaepatiwa rufaa ya kupeleka nje ya nchi,” anasema Dk Njelekela .Dk Njelekela anaongeza kuwa miongoni mwa huduma zinazofanywa katika kitengo hicho cha moyo ni upasuajai wa wa kuziba matundu kwenye moyo,kubadilisha valvu ambazo zimebana na kushindwa kuruhusu damu kupita kwenye moyo au kulegea na kufanya damu kuvuja kwenda sehemu isiyohusika na kurudisha moyo katika hali yake ya kawaida.
Dk Njelekela anasema sambamba na kitengo hicho kutoa huduma hiyo ya tiba, pia itafanya huduma nyingine ikiwamo kliniki ya magonjwa ya valve ,moyo kutanuka ,mishipa kuziba,mapigo kushuka pamoja na ugonjwa wa moyo ya kuzaliwa kwa watoto na upasuaji.
Takwimu za Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii zinaonyesha kuwa hadi Aprili mwaka huu wagonjwa 402 walisafirishwa nje kwenda kupata matibabu ambapo kati ya hao, 189 walikuwa na matatizo ya moyo, 39 saratani , 34 figo na wengine 140 magonjwa mengine .
Rufaa hiyo ilitokana na wagonjwa hao kushindwa kupata matibabu yao nchini.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo katika kituo hicho, Dk Robert Mvungi anasema kulingana na takwimu pamoja na tafiti zilizofanywa nchi inaonyesha asilimia 30 ya Watanzania wa vijijini na mjini wana matatizo ya ugonjwa wa moyo.
“Ugonjwa wa moyo umeendelea kuongezeka kwa kiasi kikubwa mjini na vijijini ambapo asilimia 30 ya Watanzania waliopo Kusini mwa Jangwa la Sahara baraniAfrika wanaugua ugonjwa huo,”anasema Dk Mvungi.
Anafafanua kuwa vyanzo vikuu vya ugonjwa wa moyo ni pamoja na unene, kuugua ugonjwa wa kisukari na mfumo wa maisha hasa kipato kinapoongezeka.
Anasema kati ya asilimia 20 hadi 30 ya Watanzania wana unene uliokithiri ambao unahatarisha afya zao na kusababisha upatikanaji wa ugonjwa wa moyo.
Anasema Dk Mvungi kuwa kulingana na kuwepo kwa viashiria vya ugonjwa huo kama ilivyoanisha, hata hivyo wagonjwa wengi wanaowasili katika kupima afya zao wanafika hospitalini wakiwa wapo katika hatua ngumu ya kupona ugonjwa huo. Anaongeza kuwa baada ya kuanza kwa kutibu ya ugonjwa huo Muhimbili, wagonjwa 453 tayari wameshafanyiwa upasuaji .
Hata hivyo, mtaalam huyo anaeleza kuwa kitengo hicho kinakabiliwa na changamoto ya upungufu wa wafanyakazi wa kada mbalimbali ,ambapo wanatakiwa wawe 365 badala ya 121 ya wataalamu waliopo sasa hali inayosababisha kukidhi mahitaji halisi ya utoaji wa huduma.
Mkurugenzi wa Fedha na Mipango ya Hospitali ya Taifa Muhimbili, Agnes Kuhenga anasema mgonjwa mwenye rufaa kutoka katika hospitali nyingine atatibiwa kwa gharama ya Sh10,000 kwa kumwona daktari, Sh20,000 kama akilazwa na Sh50,000 kama atapatiwa upasuaji.
Anasema katika kuwatibu wagonjwa hao katika kituo hicho kuna wagonjwa wa aina tatu ambapo wagonjwa wenye msamaha,wagonjwa wenye bima .Anasema kwa wagonjwa wenye msamaha kulingana na sera ya taifa,wenye maambukizi ya virusi vya Ukimwi ,wanaougua Kifua Kikuu (TB) na watoto wenye umrichini ya miaka mitano watatibiwa bure.
Anasema kwa upande wa wagonjwa wengine watakaofika katika katika kitengo hicho watatibiwa kulingana na utaratibu wa daktari husika kwa mgonjwa wake.
Na Zaina Malongo, Mwananchi
0 Comments