Dar es Salaam/Zanzibar.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko, Jaji Joseph Warioba amesema Watanzania hawatatendewa haki kama itapatikana Katiba Mpya ambayo haijatokana na maoni yao. “Hakikisheni Katiba Mpya inayopatikana ni ya maoni ya wananchi,” alisema jana muda mfupi baada ya kumaliza mkutano wake na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana.
Jaji Warioba alisema maoni yaliyomo katika Rasimu ya Katiba yametokana na maoni ya wananchi, hivyo lazima yalindwe ili kudumisha amani... “Kilichomo katika Rasimu ya Katiba ni maoni ya wananchi, wasije wakafanya makosa ya kutoa maoni haya. Haya yametoka kwa wananchi na wao ndiyo watakuwa na sauti ya mwisho kuhusu mchakato huu,” alisema na kuongeza: “Wahakikishe kwamba mawazo yaliyotolewa na wananchi yanaingia katika Katiba Mpya, wasithubutu kuyatoa maana wananchi wanaweza kukataa hali hiyo.”
Wakati Warioba akieleza hayo, viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa wameunga mkono kauli ya Jaji Warioba ya kuwataka kukaa meza moja na kuweka tofauti zao kando.
Wakati Jaji Warioba akisema hayo, vyama vya siasa vimeendelea ‘kurushiana madongo’ na kushikilia misimamo yake.
CCM kimeonya kuwa mikutano ya hadhara, maandamano au kumshinikiza Rais Jakaya Kikwete asisaini Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba mwaka 2013, si ufumbuzi wa kupatikana Katiba Mpya.
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Tanzania Bara, Philip Mangula alisema jana kwamba muswada huo ulipitishwa na wabunge kwa mujibu wa sheria baada ya wapinzani kushindwa kujenga hoja na kukimbia, hivyo kitakuwa ni kitu cha ajabu usisainiwe na kuwa sheria.
“Demokrasia ni wengi wape na wachache wasikilizwe, ikiwa wengi wameamua wana haki ya kusikilizwa na kuheshimiwa, uchache wa wapinzani hauwezi kuzuia matakwa ya wengi kukwama,” alisema Mangula.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alisema mchakato wa kudai Katiba Mpya uliozinduliwa na vyama vya upinzani hautarudi nyuma na utazidi kusonga mbele... “Tunamwomba Rais asisaini muswada huo kama kweli ana nia njema na wananchi wake na sisi haturudi katika suala hili. Tutarudisha jukumu hilo kwa wananchi waamue wenyewe.”
Naibu Katibu Mkuu wa (CUF), Julius Mtatiro alisema: “Tunaunga mkono kauli ya Jaji Warioba, lakini asiseme tuache kutumia majukwaa kuzungumzia mchakato wa Katiba kwani Katiba siyo jambo la siri.”
Alisema wanachokifanya ni kuwaelimisha wananchi ili wafahamu mambo yanayoendelea na uchakachuaji unaofanywa na CCM.
Naibu Katibu Mkuu wa NCCR Mageuzi, Samuel Ruhuza alisema, mikutano wanayoifanya isieleweke vibaya kwani wanatumia njia hiyo kuwaelimisha wananchi.“Tunachokifanya ni kuwapa elimu ili waweze kufahamu lakini siyo kutaka kuvuruga mchakato wa Katiba,” alisema Ruhuza.
|
0 Comments